ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 30, 2018

TSC yaonya walimu wanaodanganya umri wa kustaafu

Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa akiongea na walimu wakuu na wakuu wa shule (hawapo pichani) kutoka Wilaya za Bagamoyo na Chalinze. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bibi Fatuma Latu, wa kwanza kulia ni Katibu Msaidizi Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Bagamoyo, Bibi Happy Kabuka akifuatiwa na Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo Bibi, Erica Yegela.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo Bibi, Erica Yegela akiongea katika mkutano wa walimu wakuu na wakuu washule mjini Bagamoyo. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bibi Fatuma Latu (wa kwanza kushoto) akifuatiwa na Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa pamoja na maofisa wengine walioambatana nao.
Baadhi ya walimu wakuu na wakuu wa shule kutoka wilaya za Bagamoyo na Chalinze wakimsikiliza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa (hayupo pichani).
Baadhi ya walimu wakuu na wakuu wa shule kutoka wilaya za Bagamoyo na Chalinze wakimsikiliza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa (hayupo pichani)
Mmoja wa walimu akiuliza swali kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa (hayupo pichani) katika mkutano wa walimu wakuu na wakuu wa shule mjini Bagamoyo.
Mmoja wa walimu akiuliza swali kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa (hayupo pichani) katika mkutano wa walimu wakuu na wakuu wa shule mjini Bagamoyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bibi Fatuma Latu akiongea na Katibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutahindurwa (kushoto) katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.

Na Adili Mhina,
Katibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Bibi Winifrida Rutahindurwa  amewaonya waalimu wanaofanya udanganyifu katika taarifa zao za kiutumishi kwa lengo la kujiongezea muda wa kuwepo katika utumishi wa umma licha ya kuwa umri wao wa kustaafu kwa mujibu wa sheria  umefika.
Bibi Rutahindurwa alitoa kauli hiyo jana (Mei 29, 2018) mjini Bagamoyo alipokutana na waalimu wakuu na wakuu wa shule za umma kutoka wilaya za Bagamoyo na Chalinze kwa lengo la kutoa elimu juu ya wajibu wao kama mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa mwalimu kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu na. 25 ya mwaka 2015.
Alieleza kuwa kuna wakati walimu walitakiwa kupeleka taarifa zao za kiutumishi kwa waajiri wao lakini baadhi yao walipeleka taarifa tofauti na zile walizojaza kwenye mikataba ya kazi wakati wa kuanza ajira.
“Kuna baadhi ya waalimu wanajifanya hawakumbuki walizaliwa mwaka gani wakati walijaza mikataba wakati wanaaza ajira na wengi wao wamebadilisha taarifa zao na kujipunguzia umri jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sheria”. Alisema.
Alitoa ufafanuzi kuwa mwalimu atakapoandikiwa kibali cha kustaafu, TSC pamoja na mfuko wamifuko ya hifadhi ya jamii wanajikita zaidi kuangalia taarifa za mwalimu alizojaza awali wakati anaaza ajira yake na sio kutegemea taarifa za stakabadhi ya mishahara peke yake.
Bibi Rutahindurwa aliweka bayana kuwa yapo madhara kwa mwalimu ambaye muda wake wa kustaafu utafika lakini akaendelea kuwepo kazini kwa kuwa wakati wa kuchukua mafao yake atakatwa mishahara yote aliyolipwa kwa kipindi chote alichofanya kazi baada ya muda wake wa halali wa kustaafu kupita.
Alisisitiza walimu kuwa,“ naomba muwaeleze waalilmu wote katika shule zenu kuwa utakapoandikiwa kibali cha kustaafu sisi tunaangalia zaidi taarifa zako ulizojaza wakati unaajiriwa na kibainika umedanganya utachukuliwa hatua kwa kuwa umemwibia mwajiri”.
Aliongeza kuwa TSC ina taarifa zote za waalimu walizojaza wakati wakuajiriwa hivyo, kwa waalimu wote ambao hawakumbuki taarifa zao wawasiliane na ofisi za tume ya utumishi wa waalimu katika wilaya zao ili kupata uhakika wa tarehe zao za kustaafu.
Katibu huyo aliwaeleza waalimu kuwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa walimu namba 25 ya mwaka 2015, wao ndio mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa walimu. Hivyo, wanapaswa kuwashauri na kuwaelimisha waalimu juu ya kanuni na taratibu za kiutumishi badala ya kukaa na kusubiri wafanye makosa ili wawachukulie hatua.
Kwa upande wao waalimu walionesha kupokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuondoa usumbufu kwa mwalimu pale anafuatilia masuala yake ya mafao mara baada ya kustaafu.
Waalimu hao wametoa pongezi kwa katibu wa TSC kwa jitihada kubwa anazofanya katika kuhakikisha mashauri ya walimu yanafanyiwa kazi  na maamuzi yanatolewa kwa muda muafaka.

No comments: