Advertisements

Sunday, July 22, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS


Simu: +255 (0) 26 2322402-4
Tovuti:   www.tsc.go.tz

Tume ya Utumishi wa Walimu,
Mtaa wa Mtendeni,
S.L.P.  353,
DODOMA.
                                   
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WALIMU WALIOPANGIWA VITUO VYA KAZI KUZINGATIA SHERIA,  KANUNI NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA WALIMU

Kufuatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwapangia jumla ya walimu 4,840 vituo vya kazi kwenye Shule za Msingi na Sekondari nchini, Katibu  Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa amewataka waajiriwa hao kuzingatia kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wa walimu ili kujiepusha na makosa ya kinidhamu.

Amesema kuwa, kumekuwa na mazoea kwa walimu wengi kusaini nyaraka wanazopewa wakati  wa kuanza ajira bila kuzisoma kitu kinachosababisha kutoelewa kanuni na taratibu za taaluma ya ualimu katika utumishi wa Umma.

“Wapo  walimu wengi ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na wengine wamejikuta wakipoteza ajira zao kwa sababu ya kwenda kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu pamoja na zile zinazoongoza Utumishi wa Umma” amesema Bibi Rutaindurwa.


Amefafanua kuwa, Mwajiriwa atakaporipoti kwenye Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya yenye  Shule aliyopangiwa, atapewa mkataba wa ajira ulioandaliwa na Tume ya Utumishi wa Walimu. Mwajiriwa anatakiwa kusoma mkataba huo pamoja na viambatisho  vyake ili aweze kujua haki na wajibu katika utumishi wake.

“Mara nyingi  walimu wanapoajiriwa,  wengi wao wanasaini mikataba ya ajira bila kuisoma na kuelewa. Sasa naelekeza kuwa,  kila Mwalimu ahakikishe anasoma mkataba wake na anauelewa vizuri kabla hajausaini ili kujua  kwa undani kile anachotakiwa kufanya katika utumishi wake” amesema Bibi Rutaindurwa.
Ameongeza kuwa, waajiriwa wanapaswa kusoma Sheria ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Kanuni pamoja na Miongozo mingine ambayo inapatikana katika tovuti ya Tume ya Utumishi wa Walimu kupitia www.tsc.go.tz.

Wakati huo huo, Bibi Rutaindurwa amewataka Kaimu Katibu Wasaidizi Wilaya zote kuhakikisha wanatoa ufafanuzi wa mikataba pamoja na kuwaelimisha walimu walioajiriwa masuala mbalimbali yanayohusu ajira zao kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu na. 25  ya mwaka 2015.

Ameelekeza kuwa, baada ya mwalimu kukamilisha taratibu zote za kiutumishi,  Kaimu Katibu Wasaidizi watoe barua za ajira kwa waajiriwa wapya kwa wakati bila kuweka urasimu unaoleta usumbufu.

Ameongeza kuwa, hatamvumila Mtendaji yeyote wa Tume ya Utumishi wa Walimu ambaye atafanya uzembe au kuchelewesha barua za ajira kwa  Walimu bila sababu za msingi.

Mwalimu anapokamilisha kujaza nyaraka za ajira yake apewe barua ya ajira, bila urasimu wowote ili aanze kutekeleza majukumu yake kwa haraka. Sitaki kusikia mwalimu amechelewa kupata barua ya ajira au kuna mtumishi wa Tume analeta urasimu kinyume na taratibu, kwa kweli sitamvumilia” amesema Bibi Rutaindurwa.

Vilevile, amewakumbusha Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuwashauri na kuwaelimisha walimu juu ya kanuni na taratibu za kiutumishi badala ya kukaa na kusubiri wafanye makosa ili wawachukulie hatua za kinidhamu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ndio mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa mwalimu. Hivyo, walimu wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni za Utumishi wa Walimu na zile za Utumishi wa Umma.

Adili Mhina,
Afisa Mawasiliano,
Tume ya Utumishi wa Walimu.
22/07/2018.

No comments: