Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bw. Biswalo Mganga akisalimia na Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa muda mfupi kabla ya Waziri Mkuu kuzindua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, tukio lilofanyika kati kati ya wiki Jijini Dodoma. Katika taarifa yake DPP Mganga alieleza mpango wa Ofisi yake kujenga Chuo kitakachotoa mafunzo kwa Waendesha Mashtaka nchini. (Picha na Habari kwa hisani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, inakusudia kujenga Chuo cha aina yake kwaajili ya waendesha mashtaka nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo na ujuzi wa uendeshaji wa kesi na mashauri ya jinai.
Mkurugezi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, (DPP) Bw. Biswalo Mganga amesema Chuo hicho kitajengwa eneo la Usagara. Jijini Mwanza ambako tayari hekta 25 zimeshapatika kwaajili ya ujenzi huo.
Kwa Mujibu wa DPP ujenzi wa Chuo hicho unatokana na ukweli kwamba, hakuna chuo chochote kinachotoa mafunzo ya uendeshaji na usimamiaji wa kesi za jinai na kwa sababu hiyo Ofisi yake imeona kuna haja na umuhimu wa kuwapo kwa Chuo hicho.
Alikuwa akizungumza wakati hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, uliofanywa mwanzoni mwa wiki hii, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jijini Dodoma
"Mhe. Waziri Mkuu, moja ya mikakati na mipango tuliyonayo ni kujenga chuo cha aina yaka katika Afrika ya Mashariki kitakachotoa mafunzo na namna ya kuendesha kesi za jinai. Tumeshapata hati ya kiwanja chenye ukubwa wa hekta 25 eneo la Usagara Mwanza kwaajili ya ujenzi wa chuo hicho". Amebainisha Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka.
Bw. Mganga ameeleza kwamba ujenzi wa chuo huo utafanywa kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali, na kuwa sasa hivi ofisi yake ipo katika hatua za mwisho kukamilisha andiko kwa ajili ya kuombea fedha za ujenzi wa chuo hicho.
"Malengo yetu ni kuwa na chuo ambacho baadaye kitatumika kuwafundisha waendesha mashtaka kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika na baadaye Afrika kwa ujumla".
Akasema baadhi ya walimu watakao toa mafunzo hayo watakuwa ni pamoja na mawakili wa serikali ambao wamekwisha staafu na ambao wamebobea na kuwa na uzoefu mkubwa katika uendesheshaji wa kesi za jinai.
DPP ameiomba Serikali kuunga mkono ujenzi wa chuo hicho na kuhakikisha kwamba ujenzi wake unaanza mara moja.
Akielezea baadhi ya majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufuatia muundo mpya uliotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 49 la mwaka 2018 Ofisi ya Mashtaka ni huru na yenye mamlaka kamili ambayo baadhi ya majukumu yake ni pamoja na;
Kuchukua na kuendesha kesi zote za jinai kwa niaba ya Jamhuri; kuratibu na kusimamia upelelezi wa makosa ya jinai na kusimamia uendeshaji wa keshi hizo katika mahakama zote nchini, kuwasimamia mawakili wa serikali na waendesha mashtaka wote nchini na watumishi wote waliopo katika ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kumtaka mtumishi yeyote wa Serikali kutoa maelezo au taarifa kuhusiana na uendeshaji wa kesi za jinai.
Majukumu mengine ni kuchukua na kuendeleza mwenendo wa mashauri, rufaa au utekelezaji wa amri inayotokana na shauri lolote ambalo Jamhuri ina maslahi nayo na kutoa mwongozo kwa watumishi wa Umma wanaofanya shughuli zinazohusiana na uendeshaji wa mashauri ya jinai mahakamani.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameunga mkono hoja na mpango wa kujengwa kwa Chuo hicho.
Akasema Waziri Mkuu " Ofisi ya Mashtaka iendelee na mpango wake wa kupanua wigo wake wa utoaji huduma na kuboresha uelewa wa mwenendo wa mashtaka kwa kutekeleza mpango wa ujenzi wa Chuo mahususi kwa kazi hiyo".
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ni muhimu na sisi ( Tanzania) tukawahi kukijenga chuo hicho ili tupate faidia ambazo zimeainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Waziri Mkuu amesema kuwa matarajio ya kila mtanzania ni kuwa Ofisi hiyo haitotumia vibaya taratibu za utoaji haki kama vile kuchelewesha usikilizaji wa kesi au kupinga dhamana za watuhumiwa bila ya kuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo.
"Ni matumaini ya watanzania kwambma katika utekelezaji wa majukumi yenu hamtawafungulia kesi watuhumiwa bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwafungulia watuhumiwa kesi zaidi ya mara mbili au tatu bilaya kuwa na ushahidi wa kutosha hata pale ambapo watuhumiwa hao wameachiwa na mahakama." Amesisitiza Waziri Mkuu
Na kuongeza " Sanjari na hayo, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inapswa na inategemewa kuzingatia maslahi ya umma kwa kufungua na kuendesha mashtaka ambayo yana maslahi ya umma tu. Ofisi haipaswi kujishughulisha na masuala ambayo kwa ujumla wake au kwa taathira yake hayazingatii maslahi ya umma na hiyvo, kuisababishia hasara Serikali kwa maana ya upotevu wa muda na matumizi mabaya ya raslimali.
No comments:
Post a Comment