Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Kimataifa cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman uliofika Ofisini kwake Vuga kwa mazungumzo ya kuataka kuanzisha Chuo Kikuu Visiwani Zanzibar.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini humo Dr. Muneer Moh’d Al – Naamany wa Pili kutoka Kulia akielezea msimamo wa Uongozi wa Chuo chake kutaka kuanzisha Chuo Kikuu Visiwani Zanzibar.
Dr. Muneer Moh’d Al – Naamany akisisitiza jambo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Naibu Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman Dr. Ahmed Al – Naamany akimueleza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma aliyeshiriki mazungumzo hayo fursa zitakazopatikana katika mafunzo yatakayotolewa na Chuo hicho.
Dkt. Muneer Moh’d Al – Naamany akifafanua zaidi malengo ya Chuo chake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia baadhi ya vitabu vynye mfumo wa Mitaala ya Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini. Picha na – OMPR – ZNZ.
Uongozi wa Chuo cha Kimataifa cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman umekusudia kuanzisha chuo chengine kipya cha Kimataifa Visiwani Zanzibar kitachopewa jina la American and Europe of East Africa kwa lengo la kutanua Sekta ya Elimu ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini humo Dr. Muneer Moh’d Al – Naamany alitoa kauli hiyo wakati Ujumbe aliouongoza wa Chuo hicho ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Dr. Muneer Moh’d Al – Mastar alisema Zanzibar lazima iwe kituo cha Elimu katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika kitakachomjengea uwezo wa ajira ya kuaminika mahali popote Duniani Mwanafunzi aatakayemaliza masomo yake kwenye Chuo hicho.
Alisema mazingira ya kumfinyanga Mwanafunzi katika muelekeo wa chuo hicho kinachokusudiwa kuanzishwa Zanzibar unatokana na uzoefu wa miaka 20 tokea kuanzishwa kwa Chuo chao chenye Wahadhiri kutoka pembe zote za Dunia wanaofundisha kwenye Taasisi yao.
Mkuu huyo wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Oman mwenye Asili ya Zanzibar alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Chuo chake umefikiria Mpango huo kwa nia ya kuirejeshea hadhi yake Zanzibar kuwa Kituo cha masuala mengi katika enzi zilizopita hasa harakati za Biashara na usafiri uliokuwa ukiunganisha Dunia.
Naye kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman Dr. Ahmed Al – Naamany alisema mfumo wa ufundishaji utakaotumika utampa uwezo Mwanafunzi kuendelea na masomo yake hata akiwa nje ya Zanzibar.
Dr Ahmed alisema Mwanafunzi hata akiwa Dar es salaam, Nairobi au sehemu yoyote ya Afrika ya Mashariki ataweza kuunganishwa katika mfumo wa mafunzo ya Mtandao wa Teknolojia ya Kisasa akienda sambamba na Wanafunzi wenzake watakaokuwa darasani.
Naibu Mkuu huyo wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mwanafunzi atakayemaliza mafunzo yake atauzika bila ya wasi wasi katika Taasisi zozote zile iwe za Kitaifa au hata Kimataifa.
Akitoa ufafanuzi kwa Ujumbe huo wa Oman Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma alisema wazo la Uongozi wa Chuo hicho cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman ni fursa nzuri kwa vile imelenga kuimarisha Sekta ya Elimu.
Mh. Riziki alisema katika kuunga mkono mawazo hayo vipo vyuo vilivyo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA} ambavyo Uongozi huo unaweza kuangalia mazingira yake iwapo utapatikana uwezekano wa kuunganishwa katika muelekeo walioukusudia.
Hata hivyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar alieleza kwamba Wizara yake inayachukuwa mawazo hayo kwa kuyafanyia kazi mara moja ili baadaye kuyawasilisha Serikalini kwa hatua sambamba na maamuzi muwafaka.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuupa fursa Uongozi huo kuanzisha Chuo chake Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif alisema kinachohitajika hivi sasa kwa Uongozi huo ni kuandika maombi rasmi na kuyafikisha Serikalini kwa hatua itakayostahiki ili ile azma yao ya kutanua Sekta ya Elimu ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki iweze kufanikiwa vyema.
Uongozi wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman endapo utapata fursa hiyo umelenga kuanza mradi wao wa Chuo mapema Mwezi Septemba Mwaka ujao was 2019 hata kwa kuanza na majengo ya muda.
No comments:
Post a Comment