ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 31, 2018

Waziri Hasunga aziagiza Bodi za Mazao nchini kuwasajili Wakulima wote

Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma jana tarehe 29 Disemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akifatilia mkutano wa Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao,  uliongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma jana tarehe 29 Disemba 2018.
Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao,  wakifatilia mkutano wa kazi ulioongozwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (Mb) kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma jana tarehe 29 Disemba 2018.

Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (Mb)  amewaagiza Wakurugenzi wa Bodi za Mazao kuanza mara moja zoezi la kuwatambua na kuwasajili wakulima wa mazao yote nchini lengo likiwa kuwatambua ili kupanga mipango sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote.

Ametoa agizo hilo jana tarehe 29 Disemba 2018 wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma.

Mhe. Hasunga amesema ili kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza mazao yote ni vyema kuwatambua Wakulima wote nchini na kuongeza kuwa Wakulima wa zao la korosho wametoa funzo kubwa kwa  Wizara yake kufanya jambo kama hili katika mazao mengine hapa nchini.

Itakumbukwa kuwa wiki tatu zilizopita, Waziri Hasunga alitoa agizo kwa Bodi ya Korosho agizo kuandaa daftali maalumu la kuwatambua Wakulima wa korosho kote nchi ambapo moja ya taarifa ambazo zitajumuishwa katika daftali hilo ni pamoja na Jina Kamili la Mkulima,  Mkoa, Wilaya, Kata na Tarafa anayotoka.

Mambo mengine ni pamoja na Kitongoji, Mtaa au Jina la Kijijini anapotoka, mahali lilipo shamba pamoja na ukubwa wa shamba lake.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa mipango sahihi ya kuwaendeleza Wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia katika hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko ni vyema kuwa na mfumo maalumu wa kanzi data (Database) ya kuwafahamu ili kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi.

Waziri Hasunga alienda mbali na kushauri matumizi ya TEHAMA na ya Mfumo wa GPS ili kuboresha daftari hilo kwa lengo la kuboresha uwekaji wa taarifa za Wakulima na maeneo wanayotoka Wakulima kwa usahihi zaidi.

“Tumepata changamoto kadhaa wakati wa kuwahakiki Wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma na kama Bodi ya Korosho ingekuwa makini kuandaa daftari la Wakulima zoezi la uhakiki lingekuwa rahisi, kwa ajili hiyo niliwaagiza Bodi ya Korosho kukamilisha zoezi hili mpaka Mwezi Machi, 2019 na Bodi za Mazao zilizobaki ukiacha Bodi ya Tumbaku ambao wao tayari walishafanya hivyo, kukamilisha Mwezi June, 2019”. Amekaririwa Mhe. Hasunga.

Waziri ameitisha kikao maalumu na Viongozi wa Bodi za Mazao, Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuboresha mikakati na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Wizara pamoja na kujitathmini kabla ya kufikia nusu mwaka wa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya Wizara ya mwaka 2018/2019 ili kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya kilimo ya mwaka ujao wa 2019/2020.

Bodi za Mazao zilizoshiriki mkutano huo ni pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Mkonge, Bodi ya Pareto, Bodi ya Chai, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Bodi ya Sukari.

Wakala zilizoshiriki ni pamoja na  Wakala wa Taifa wa Mbolea (ASA) Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA).

Taasisi nyengine za Wizara ya Kilimo zilizoshiriki ni pamoja na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) na Bodi ya Leseni za Maghala.

No comments: