Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia), akimpongeza Mama Chausiku (mwenye fulana ya njano), baada ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba yake (inayoonekana pichani), akiwa katika ziara ya kazi kijijini Ibili, Wilaya ya Uyui, Desemba 14, 2018.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mbele-kulia) na Ujumbe wake, wakielekea kwenye moja ya makazi ya wananchi wa kijiji cha Ibili, wilayani Uyui kuwasha umeme. Wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba ya mkazi wa kijiji cha Ibili wilayani Uyui, Mama Chausiku (mwenye fulana ya njano), Desemba 14, 2018. Kulia kwa Waziri ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya na wa kwanza kulia ni Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almasi Maige.
Viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Umeme Vijijini wilayani Uyui, wakiwa wamesimama mbele ya wananchi wa kijiji cha Ibili kwa utambulisho maalumu wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Desemba 14, 2018.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya (aliyesimama), akimkaribisha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (anayesaini kitabu) mkoani Tabora alipofika kwa ajili ya ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Desemba 14, 2018.
Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almasi Maige, akimkaribisha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia-walioketi) mkoani Tabora alipofika kwa ajili ya ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Desemba 14, 2018.
Sehemu ya umati wa wananchi wa Kijiji cha Ibili, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Desemba 14, 2018.
Na Veronica Simba – Tabora
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekemea kasi duni ya Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora na kumtaka ndani ya siku 30 awe ameunganisha umeme vijiji vingine vipya 15. Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibili wilayani humo, Desemba 14, 2018, alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Waziri Kalemani alimwagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa eneo hilo kumwandikia barua ya onyo la kukusudia kusitisha mkataba Mkandarasi husika endapo atashindwa kutekeleza agizo alilompa.
“Na siyo kusitisha tu; tukisitisha mkataba maana yake hatutakupatia kazi tena na tutakudai malipo ambayo tumekwishakulipa na hata kukupeleka mahakamani. Nataka kasi iongezeke maradufu,” alisisitiza Waziri. Aidha, Waziri aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu kwa kuwa ni huduma inayotolewa kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) huku akiwatahadharisha kuwa muda wa kutekeleza mradi huo ukipita watalazimika kulipia gharama kubwa zaidi.
Vilevile, aliwataka pindi wakishaunganishiwa umeme, wautumie kwa malengo ya kukuza vipato vyao na kuboresha maisha ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao wanayolima ambayo ni karanga, pamba na tumbaku. Pia, aliwataka viongozi wa taasisi zinazotoa huduma kwa umma kama shule, vituo vya afya, masoko, polisi, mitambo ya maji, makanisa, misikiti, kutenga pesa na kulipia kiwango hicho cha shilingi 27,000 tu ili kuhakikisha taasisi zao zinaunganishiwa umeme hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Nawaomba sana viongozi mtekeleze hilo, maana huwa inasikitisha sana pale unapokuta nguzo zimepita mbele ya taasisi fulani lakini taasisi yenyewe haina umeme, Ukiuliza unaambiwa hawajalipia,” alifafanua. Waziri Kalemani aliwashauri wananchi na taasisi za umma kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa wale wasio na nyumba kubwa au matumizi makubwa ya umeme, kwani wataepukana na gharama za kutandaza nyaya katika majengo yao.
Sambamba na hamasa hiyo, Waziri alimkabidhi Mbunge wa Jimbo hilo, Almasi Maige vifaa 250 vya UMETA akisema ni kufuatia maombi yake kwa Waziri na pia akamwongezea vifaa vingine 15 zaidi alivyovitoa kama zawadi kwa wananchi wa eneo hilo. Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani alifuatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Almasi Maige, viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TANESCO, REA na Chama Tawala CCM.
Waziri Kalemani anaendelea na ziara yake katika mikoa mbalimbali kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo atakuwa Singida Desemba 15.
No comments:
Post a Comment