KAMA ni filamu unasema limefikia mwisho na ubao kusomeka ‘The End’. Ni kuhusu ishu ya kipa Beno Kakolanya wa Yanga aliyekuwa kwenye sintofahamu Jangwani akishinikiza kulipwa chake.
Kipa huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea Prisons misimu mitatu iliyopita, inaelezwa kuwa kwa sasa anajiandaa kutua Msimbazi na kuitumikia baada ya kesi yake ya mabosi wake kukosa suluhu mpaka sasa.
Tangu kipa huyo alipoigomea kambi akitokea Taifa Stars iliyokwenda Lesotho na Kocha Mwinyi Zahera kumfungia vioo, amekuwa kipambana aachane na wababe hao wa Jangwani ili atafute maisha kwingine bila mafanikio.
Akimtumia Mwanaseheria wake, Leonard Richard katika sakata hilo ili aweze kulitatua kwa kutumiana barua za majibishano ya kisheria kati ya viongozi wa Yanga, goma limebuma na Kakolanya anatimka.
Mwanasheria huyo alikaririwa na Mwanaspoti kuwa sakata hilo lilikuwa hatua ya mwisho kwa kupeleka barua Shirikisho la Soka Tanzania TFF) ili mchezaji huyo apate ufumbuzi wa haraka katika kuokoa kipaji chake baada ya kuwa nje muda mrefu.
Wakati Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji ikisubiriwa kutoa ufumbuzi wa sakata hilo, Mwanaspoti lilidokezwa Kakolanya amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na Simba ili kwenda kumpa changamoto Aish Manula.
Mwanaspoti lilidokezwa kuwa mmoja wa viongozi katika Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, amekuwa akiwasiliana na kipa huyo ili kukamilisha dili hilo, lakini Kakolanya anawazungusha kutokana na kutokuwa na jibu kamili kuhusu hatma yake Yanga.
“Simba kweli wanamhitaji na huyu kiongozi amekuwa akitaka kuonana na Kakolanya, lakini jamaa amekuwa akiwakwepa, lakini baadaye aliwaambia anaogopa kusaini kwani bado hajapata ufumbuzi TFF,” kilisema chanzo hicho.
Naye Kakolanya alipotafutwa na Mwanaspoti kutaka kujua msimamo wake, alisema kazi yake ni kucheza soka, hivyo kama kuna timu inamhitaji basi inatakiwa impe pesa yake ya usajili ili kuepukana na utata katika mambo ya kazi.
“Nategemea mpira ndio uendeshe maisha yangu na sio kitu kingine chochote, kwa hiyo kama kuna timu inanihitaji inabidi tumalizane mapema na iwepo kwenye mkataba ili nibaki na kazi ya kucheza tu sio kudai madeni, sipendi kuonekana jeuri mbele ya macho ya watu” alisema.
Kuhusu ishu ya kuhusishwa kujiunga na Simba, Kakolanya aligoma kabisa kuongelea suala hilo na kusema tusubiri muda ufike.
YANGA WAFUNGUKA
Mwanaspoti halikuishia hapo kwani lilimtafuta Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Samuel Lukumay kuweza kuzungumzia sakata la mchezaji huyo, alisema suala hilo halipo mikononi mwao.
“Suala la Beno tumemuachia mwanasheria wetu analisimamia kwa sasa hivyo, siwezi kulizungumzia,” alisema kwa kifupi.
No comments:
Post a Comment