ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 20, 2019

WATUMISHI WA SERIKALI WANAODAIWA KODI YA ARDHI KUSHTAKIWA

 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt. Angeline Mabula akimuagiza Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ukerewe Tewe Shaban kuwa na usimamizi mzuri wa makusanyo ya Kodi ya pango la ardhi na kuwa mfumo mzuri wa uhifadhi wa nyaraka za ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt. Angeline Mabula akiongea na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
  Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt. Angeline Mabula wakati alipofanya ziara katika wilaya hiyo. Picha zote Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt. Angeline Mabula akimuagiza Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ukerewe Tewe Shaban kuwa na usimamizi mzuri wa makusanyo ya Kodi ya pango la ardhi na kuwa mfumo mzuri wa uhifadhi wa nyaraka za ardhi. Picha zote na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi.

Na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt. Angeline Mabula ameagiza kuanza mchakato wa kuwaorodhesha watumishi wa umma ambao hawajalipa kodi ya pango la ardhi hadi sasa ili wafikishwe katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba.

Dkt. Mabula ameyasema hayo alipofanya ziara katika Wilaya ya Bunda na Serengeti mkoani Mara na wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wakati wa ziara yake inayoendelea ya kuhamasisha malipo ya kodi ya pango la ardhi  katika kanda ya ziwa.

“Nyinyi watumishi wa Serikali mnatakiwa kuwa wa mfano katika kulipa kodi za serikali kwa sababu hatuwezi kwenda kudai wengine wakati sisi wenyewe hatujalipa kodi ya pango la ardhi, na kokote ntakapopita nataka majina ya watumishi ambao hawajalipa ili wafikishwe katika mabaraza” alisisitiza Dkt. Mabula.

“Mheshimiwa Rais anasimamia miradi mikubwa hapa nchini kama ule wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa Mto Rufiji, Stiegler's Gorge na uimarishaji wa Shirika la Ndege la Tanzania ambayo miradi hii yote inategemea kodi na mapato ya ndani, hivyo ni lazima tumuunge mkono katika kulipa kodi hizi” aliongeza Dkt. Mabula.

Wakati akiwa Wilayani Ukerewe alipokea taarifa ya afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Tewe Shaban kuwa hadi sasa halmashauri yake imeshakusanya jumla ya Tsh 41,288,175 wakati lengo ni 100,000,000 kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ambayo ni sawa na 41.2% iliyokusanywa.

Afisa huyo alimueleza Dkt. Mabula kuwa hadi sasa jumla ya ilani 131 zenye thamani ya Tshs 54,446,550 za madai ya kodi ya ardhi zimesambazwa kwa wadaiwa kodi ya ardhi ambao wameanza kupunguza madeni yao na mpaka sasa wameshalipa Tshs. 3,100,700 na kubaki Tshs. 51,345,850.

Baada ya kupokea taarifa hiyo Dkt. Mabula alishangazwa na ukusanyaji huo hafifu wa maduhuli ya Serikali na alimuagiza Afisa huyo kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo, na aanze na watumishi wote wa Serikali katika halmashauri ya wilaya ya Ukerewe.

Katika kuhakikisha linatekelezwa hilo Dkt. Mabula akaagiza kuwepo kwa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi atakayesimamia kesi hizo na kuzitolea hukumu kwa wadaiwa sugu waweze kulipa kwa wakati na kama hawatotekeleza basi milki zao zitauzwa ili kulipwa deni hilo.

Akiwa wilayani Bunda Dkt. Mabula alimuagiza afisa ardhi mteule kumfikishia majina ya maafisa wa halmashauri ya wilaya ya Bunda ambao wanadaiwa kodi ya pango la ardhi na hawajalipa hadi sasa wakati muda wa kulipa kwa hiari ushaisha tangu tarehe 31 januari 2018.


Vivyohivyo Dkt. Mabula akiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Serengeti amamuagiza Afisa Ardhi Mteule kukabidhi majina ya watumishi wa umma ambao wadaiwa wa kodi ya ardhi kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo ili waweze kufikishwa katika baraza ardhi iwapo watakuwa hawajalipa.

No comments: