Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi,walipowasili katika Gereza la Wanawake Kingolwira Mkoani Morogoro kuzungumza na wafungwa ikiwa ni ziara ya kufuatilia utekelezaji wa serikali.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Jumla ya wafungwa na mahabusu 15,250 nchini wamepima Virusi vya Ukimwi huku 340 wakikutwa na maambukizi baada ya Jeshi la Magereza wakishikiana na Wizara ya Afya kutoa elimu ya Upimaji katika Magereza mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akiwasilisha Taarifa Kuhusu Hali ya Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Upatikanaji wa Tiba ya Magonjwa Nyemelezi na Udhibiti wa Biashara na Matumizi ya Dawa za Kulevya Magerezani kwa mwaka ulioisha.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI iliyofika katika Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira mkoani Morogoro, Naibu Waziri Masauni alisema kati ya mahabusu na wafungwa waliopima wanaume waliokutwa na maambukizi ni 292 na wanawake ni 48
“Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Afya wanahakikisha huduma za afya zinaboreka magerezani ikiwemo lishe nzuri kwa wanaothibitika wana maambukizi huku jumla ya wafungwa na mahabusu wanaotumia dawa za kufubaza makali wakiwa 1,496” alisema Naibu Waziri Masauni
“.. elimu ya kifua kikuu na upimaji inatolewa kila siku Magerezani kwa wafungwa na mahabusu, kwa mwaka jana jumla ya waliopima ni 12,870 huku waliobainika na maambukizi ni 167 na tunashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kwa kuandaa Mpango Mkakati wa UKIMWI na kifua Kikuu kwa miaka mitano.” Aliongeza Masauni
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuwatembelea wafungwa katika Gereza la Kingolwira Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI , walilipongeza Jeshi la Magereza kwa kuwahudumia mahabusu na wafungwa wanaoishi na maambukizi magerezani huku wakitoa wito kwa wafungwa walioathirika kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao kuhusiana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Afya na Lishe wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Dkt.Hassan Mkwiche alisema magereza yana utaratibu wa kupima afya za mahabusu au wafungwa siku ya kwanza tu anayoingia gerezani ikiwemo ujauzito, Ukimwi, kifua kikuu na magonjwa mengine ili waweze kuhudumia kila mfungwa na mahitaji yake.
“Mfungwa anapoingia humu anaenda kukutana na kazi mbalimbali kwahiyo ni muhimu kujua afya ya kila mmoja tangu siku ya kwanza anaingia ili kuweza kumpangia majukumu kulingana na afya yake lakini pia aina ya mlo anaotakiwa ale akiwa kifungoni” alisema Dkt. Mkwiche.
Juhudi mbalimbali za kuboresha afya za wafungwa magerezani zinaendelea huku Wizara ikiendelea kuboresha vituo vya kutoa huduma za afya ambapo mwaka 2018 zahanati ya Gereza Mahabusu mkoani Morogoro ilikamilika na imeshaanza kufanya kazi huku gharama za ujenzi zikiwa ni fedha za ndani za serikali.
No comments:
Post a Comment