Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Soka ya Ujamaa Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Seti Tano za Jezi Mwenyekiti wa Klabu hiyo Mohamed Makame Machano kutekeleza ahadi aliyoitoa alipoitembelea Klabu hiyo Mwaka 2018. Anayeshuhudia tukio hilo wa kwanza kushoto ni Mzee wa Klabu ya Ujamaa Mzee Ameir Makungu.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kulia akiukumbusha Uongozi wa Klabu ya Ujamaa kuhakikisha kwamba Vijana wao wanazingatia nidhamu katika mazoezi yao ili kuijengea sifa Klabu hiyo. Picha na – OMPR – ZNZ.
Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Soka ya Ujamaa yenye mastakimu yake Mtaa wa Rahaleo Mjini Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameukumbusha Uongozi wa Klabu hiyo kuendelea na jukumu lake la kuwafinyanga vyema vijana wao ili wafikile lengo walilokusudia.
Alisema hatua hiyo mbali ya kuirejeshea hadhi yake Klabu hiyo iliyokuwa nayo katika nyanja ya soka Visiwani Zanzibar lakini pia itatoa nafasi kubwa zaidi ya kuwajengea njia ya maisha bora Vijana wao katika fursa za ajira kupitia Sekta hiyo ya Michezo.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mlinda Mlango mahiri ya Ujamaa Spots Club zamani maarufu ikijuilikana kwa jina la Worlves alitoa kumbusho hilo wakati akiukabidhi Uongozi wa Timu hiyo Seti Tano za Jezi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga akitekeleza ahadi aliyoitoa kwa Timu hiyo wakati alipoitembelea Mwaka jana.
Mchezaji huyo wa zamani wa Ujamaa Sports Club ambae aliahidi pia kutoa Seti nyengine Tano kwa Timu hiyo kabla ya kumalilika kwa Mwaka 2020 alisema Mchezo wa soka hivi sasa ni ajira inayowajengea mazingira bora ya kimaisha wachezaji ambao wamejikubalisha kujifunza kwa kina mchezo huo maarufu Duniani.
Alishauri kwamba Uongozi huo wa Ujamaa lazima uhakikishe kwamba Vijana wao wote waliokubali kujisajili na Timu hiyo wanaendeleza nidhamu mchezoni kwa kufanya mazoezi kwa juhudi ili iwawezeshe kupata mafanikio makubwa.
Balozi Seif pia alitumia nafasi hiyo kuupa pole Uongozi, Wachezaji pamoja na Jamaa wa Familia ya Mchezaji wa Zamani wa Timu hiyo Marehemu Nassor Mashoto aliyefariki Dunia Tarehe 24 Januari Mwaka huu wa 2019.
Alisema Marehemu Nassor mbali ya kuiletea sifa Timu yake ya Ujamaa lakini pia aliacha athari kubwa kwa wapenda soka wakati akiichezea Timu ya Taifa ya Soka ya Zanzibar katika kipindi cha umahiri wake alipokuwa dimbani.
Balozi Seif alisema msiba huo haukuwa wa Uongozi wa Timu, Wachezaji pamoja na Familia bali uliwagusa wanasoka wote wa Visiwa vya Zanzibar, Tanzania, Afrika ya Mashariki na hasa katika Mji wa Mombasa Nchini Kenya.
Akitoa shukrani wakati akipokea msaada huo wa seti Tano za Jezi kwa niaba ya Uongozi na Timu ya Soka ya Ujamaa Mwenyekiti wa Timu hiyo Mohamed Makame Machano alisema Vijana wa Timu hiyo hivi sasa wanaendelea vyema katika mashindano yao ya Daraja la Pili.
Mohamed alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Klabu hiyo umepata faraja kubwa kutokana na Vijana wao kufanya vyema ndani ya msimu huu unawajengea mazingira ya kusonga mbele kutokana na nafasi waliyonayo katika muendelezo wa mashindano yao.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Klabu ya Ujamaa iliyopo Mtaa wa Rahaleo alimuomba Mchezaji huyo wa zamani wa Klabu hiyo kufikiria wazo la kuwapatia Viatu wachezaji wao ili kuwajengea hadhi bora zaidi hasa wakati wanapokuwa kwenye mashindano.
Ujamaa ni miongoni mwa Timu kongwe za Soka Visiwani Zanzibar iliyojipatia umaarufu mkubwa kutokana na Historia yake za kusakata kabumbu lililopelekea kutoa wachezaji kadhaa wa Timu ya Taifa ya Zanzibar kwenye Mashindano ya Challenge kwa wakati huo yakiitwa Gorsage.
No comments:
Post a Comment