ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 15, 2019

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa mahakama

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.) wakati Kamati hiyo ya Bunge ilipokuwa ikikagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa mahakama Mkoani Mbeya.  “Kamati inaipongeza Wizara ya Katiba na Sheria na Uongozi wa Mahakama kwa kusimamia kwa weledi miradi ya mahakama hapa nchini.” Aliendelea kusema “Kamati inawasihi (Wizara na Mahakama) kuhakikisha mnakamilisha miradi hiyo kwa kuzingatia muda uliopangwa na viwango vyenye ubora uliothibishwa.” Alisema Mheshimiwa Mchengerwa. 

Mheshimiwa Balozi Augustine Mahiga (Mb.), Waziri wa Katiba na Sheria ameambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya ziara ya siku tano (13-17 Machi 2019) ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa mahakama hapa nchini. Ziara hiyo ni ya kwanza tangu Balozi Mahiga alipokabidhiwa rasmi Wizara hiyo tarehe12 Machi 2019 na Mheshimiwa Waziri Profesa Palamagamba Kabudi (Mb.) aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akieleza ushiriki wa Waziri Mahiga kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati alieleza kuwa, ni Waziri wa kwanza kuambatana na Kamati hiyo katika ukaguzi wa miradi ya mahakama tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani. Alieleza kuwa, Kamati yake imefarijika sana na kitendo hicho na kuahidi kwa niaba ya Kamati kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali.   
Akitoa taarifa ya ujenzi wa miradi hiyo, Waziri Mahiga alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/19 Mahakama imeendelea kutekeleza miradi 35 ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Alieleza kuwa, pamoja na kukagua miradi ya Mkoa wa Mbeya,  Kamati hiyo itaendelea na ziara ya kujihakikishia utekelezaji wa miradi hiyo kwenye Mkoa wa Njombe, Arusha, na Manyara kabla ya kuanza Mkutano wa 15 wa  Bunge la Bajeti tarehe 2 Aprili 2019.
Alieleza kuwa, kwa mwaka huo wa fedha Mahakama ilitengewa kiasi cha Tshs. 35,973,722,000/= ikiwa ni fedha za maendeleo. Kati ya fedha hizo Tshs. 15,000,000,000/= ni fedha za ndani na Tshs. 20,973,722,000/= fedha za nje. Kati ya fedha zote za ndani Bilioni 5 imeshatumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama, Bw. Solanus M. Nyimbi alieleza kuwa, katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo kumekuwa na changamoto kadhaa hususan mtiririko wa fedha za maendeleo; mazingira: jiografia ya eneo, hali ya hewa na aina ya udongo katika maeneo ya mradi; na changamoto za umiliki wa viwanja hususan katika miradi viporo. Alieleza kuwa, pamoja na changamoto hizo wameendelea kujitahidi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa. 

No comments: