ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 4, 2019

MAKAMU WA RAIS AFANYA ZIARA USHETU WILAYANI KAHAMA

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Ezekiel Maige mara baada ya kuwasili kwenye kituo cha afya Ngaya wilayani Kahama, Shinyanga. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha afya Ngaya wilayani Kahama, Shinyanga. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimu wajasiriamali katika eneo la Bukondamoyo wakati akiwa njiani kuelekea Ushetu, Kahama mkoani Shinyanga. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi wa Ushetu katika uwanja wa Mikutano Nyamilongo wilayani Kahama, Shinyanga. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amewapongeza wananchi wa Jimbo la Ushetu kwa kupanda miti na kuvuka lengo lililowekwa kwa kila Halmashauri nchini.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika uwanja wa mikutano wa Nyamilangano, jimbo la Ushetu, wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

“Ninamuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba kufika ushetu na kuona namna bora ya kusaidia kutunza mazingira haswa kwa wakulima wa Tumbaku na kuona njia ipi bora ya kutumia mabani ya kuni kidogo ama mabani ya kutumia solar ama umeme wa kawaida” alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais ambaye leo amehitimisha ziara yake ya siku 5 yenye lengo la kuhamasisha na kukagua shughuli za maendeleo mkoani Shinyanga ambapo amefanya ziara katika wilaya zote 3.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais amehimiza wananchi wa Ushetu kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ambapo amewahakikishia kuendelea kutimiza ahadi zilizotolewa kwenye ilani ya Uchaguzi.

Aidha amewataka wananchi hao kuhakikisha watoto wao wanaepukana na mimba za utotoni na wasisite kuchukua hatua za kisheria pale inapotokea.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Innocent Bashungwa amesema Serikali ina mpango wa kujenga soko la Kimataifa la Mazao katika wilaya ya Kahama ili kufungua fursa zaidi ya wakulima kuuza mazao yao.

Pia amewahakikishia wakulima wa Tumbaku kuwa Serikali inawatafutia masoko mengine ili wawe na soko kubwa la kuuza zao hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Serikali inachimba visima 24 katika jimbo la Ushetu lakini pia inaleta mradi mkubwa wa maji yanayotoka ziwa Victoria.

No comments: