Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wahitimu 21 wa kozi ya ukalimu yanayotolewa bure kupitia mradi wa Trade Aid katika mji mkongwe wa kihistoria wa Mikindani uliopo katika Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara ambapo Mhe.Kanyasu amewataka wahitimu hao mara watakapoajiriwa waende wakaoneshe utofauti wakawe mfano bora kwa kuchochea utalii katika mikoa ya Kusini.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi waliohitimu mafunzo ya ukarimu kwa msaada wa Shirika la Trade Aid la Marekani katika Mji wa Kihistoria wa Mikindani mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akimsikiliza Salum Kidume alimpotembelea nyumbani kwake Mikindani mkoani Mtwara akimuelezea kuhusu alimvyompokea Hayati Mwl. Julius Nyerere mnamo mwaka 1950 wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.
Baadhi ya wanafunzi wakiimba kwa furaha mbele ya Naibu Waziri wa Maliasilia na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati wa mahafali yao mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akikabidhi cheti cha kuhitimu kwa Jum Abdallah ambaye ni mhitimu wa kozi ya ukalimu katika chuo cha Old Boma Mikindani mkoani Mtwara
Baadhi ya wazazi pamoja na wananchi walioshiriki katika mahafali ya 38 yaliyofanyika katika jengo la kihistoria la Olda Boma wakati wahitimu 21 walipohitimu kozi ya Ukarimu yaliyofanyika mkoani Mtwara. (PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA)
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewanyoshea kidole baadhi ya wahitimu wa masomo ya utalii wanaoajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini wanaoshindwa kutafsiri vyeti na elimu waliyoipata vyuoni kwa kutoa huduma bora kwa watalii nchini.
Amesema bado kuna tatizo la watoa huduma wengi katika maeneo ya hoteli ambao ni wavivu, wasiojituma,wenye kukosa ubunifu na wasiotumia lugha nzuri kwa watalii.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 38 kwa wahitimu 21 wa kozi ya ukarimu yanayotolewa bure kupitia mradi wa Trade Aid, kwenye mji mkongwe wa kihistoria wa Mikindani uliopo katika Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara, Mhe.Kanyasu amewataka wahitimu hao pindi watakapoajiriwa waoneshe utofauti na kuwa mfano bora kwa kuchochea utalii katika mikoa ya Kusini.
Amesema mradi huo wa Trade Aid umekuwa ukitoa mafunzo hayo kwa muda wa miezi sita kwa wanafunzi wenye elimu mchanganyiko kuanzia darasa la saba na kuendelea lengo likiwa kuisaidia jamii ya Mikindani kuchangamkia fursa za utalii.
Aidha, wanafunzi wanaohitimu mafunzo hayo kila mwaka huajiriwa moja kwa moja kwenye sekta ya hoteli nchini kutokana na ubora wao. Amesema watalii wengi wanaokuja nchini ni matokeo ya huduma bora na pale inapotokea wamehudumiwa vibaya hawawezi tena kurudi.
Hata hivyo, Mhe Kanyasu amesema licha ya kuwa kuna vyuo vingi vinavyotoa mafunzo hayo kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada, bado watoa huduma walio wengi wamekuwa na uwezo mdogo wa kuwahudumia watalii kwa viwango vya juu ikilinganishwa na elimu waliyonayo.
Amesema licha ya wafanyabiashara kujenga Hoteli za kitalii katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuwapata watoa huduma wenye uwezo wa kutoa huduma bora za kumfanya mtalii aongoze siku za kukaa nchini kutokana na huduma alizopata.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Mikindani, Mhe. Elias Mwanjise akizungumza wakati wa mahafali hayo ametoa wito kwa wahitimu hao pindi watakapojiriwa wafanye kazi kwa bidii na maarifa ya hali ya juu hali itakayopelekea watalii wengi kuja nchini.
Pia amewataka wazazi wasiwaozeshe binti zao wanaomaliza darasa LA saba na badala yake wachangamkie fursa hiyo ambayo ni nadra kupatikana katika maeneo mengine. Naye Meneja wa Mradi wa Trade Aid nchini Tanzania,Barnabas Mwambe amemweleza Naibu Waziri Mhe. Kanyasu kuwa wahitimu wanaomaliza katika Chuo hicho karibu wote wamekuwa wakiajiriwa kutokana na ubora wao na jinsi walivyoandaliwa.
Amebainisha kuwa mkazo waliouweka Chuo hapo ni mafunzo kwa vitendo kuliko nadharia ili kuwajengea uwezo wahitimu kutoa huduma bora. Mbali ya kutoa mafunzo hayo bure, Meneja Mradi huo amesema kuwa wamekuwa wakiwafungulia akaunti za benki pamoja na kuwawekea kiasi cha shilingi 150,000 kwa ajili ya nauli wakati wakitafuta kazi pamoja na kupewa kadi ya mafao uzeeni
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Husna Ally akizungumza wakati wa mahafali hayo amesema baada ya kuhitimu mafunzo ameanza kuona mwanga wa maisha kutokana na elimu ya darasa la saba aliyokuwa nayo.
No comments:
Post a Comment