Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Walimu pamoja na Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Sekondari Kinyasini alipofanya ziara fupi skulini hapo Miaka michache iliyopita na kuahidi kusaidia Kompyuta.
Balozi Seif akiangalia mabadiliko makubwa ya majengo ndani ya Skuli ya Sekondari ya Kinyasini ambapo ndipo alipoanzia kupata elimu ya msingi katika miaka ya 46.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi akizunguma na wazazi, kamati ya skuli, walimu na wanafunzi wa
skuli ya Sekondari ya Kinyasini kipindi alipofika kuona maendeleo na
changamoto zinazoikabili Skuli hiyo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi
msaada wa Laptop Mbili kwa ajili ya matumizi ya kimasomo Kwa Walimu na
Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kinyasini iliyopo Wilaya ya
Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati alipofanya ziara kipindi
cha nyuma ya kukagua na kuangalia maendeleo na changamoto
zinazoikabili skuli hiyo na kuzungumza na Uongozi wa Kamati ya Skuli,
walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Skuli hiyo.
Akipokea Msaada huo uliowasilishwa na Msaidizi wa Makamu wa Pili wa
Rais anayesimamia masuala ya Ustawi Bibi Siti Abass, Mwalimu Mkuu wa
Skuli ya Sekondari Kinyasini Mwalimu Kombo Ali Machano alisema msaada
huo umeleta ukombozi kubwa kwao na watalazimika kuutunza ili uweze
kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.
Hata hivyo Mwalimu kombo aliomba iwapo utakuwepo uwezekano wa kupatiwa
Printa itakuwa ni jambo la faraja litakalowawezesha kuweputa matatizo
yanayojitokeza wakati wanapoamua kwenda ku\ichapisha kumbukumbu zao
kwenye Kompyuta za nje.
Akielezea furaha yake Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Skuli ya
Kinyasini Bwana Is-haka Vuai Kidawa alisema Uongozi wa Skuli hiyo,
Wazazi na Wanafunzi bado wanaamini kwamba Kiongozi huyo kamwe hatosita
kuendelea kusaidia nguvu za kuimarisha Elimu Skulini hapo.
Bwana Is-haka alisema Wananchi wa Kijiji hicho na vitongoji vyake
wanaelewa kwamba Kiongozi huyo wa Juu Serikalini akiwa ndie Mtendaji
Mkuu wa Serikali amekuwa akikabiliwa na ahadi nyingi na ukweli
usiopingika kwamba inakuwa vigumu kuzitekeleza kwa wakati jambo ambalo
wao walilazimika kufanya subra kutokana na ahadi yao hiyo.
Wakati wa ziara yake Skulini hapo Miaka michache iliyopita Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Wazazi wana wajibu na
ulazima wa kuhakikisha kwamba watoto wao wanawasimamia vyema katika
kupata elimu bora itakayotoa mwanga wa kimaisha katika hatma yao ya
baadaye.
Balozi Seif alisema elimu ndio ufunguo pekee pekee utakaowapa njia
watoto hao kukabiliana na mazingira ya kimaisha yanayokwenda kwa kasi
na haraka ndani ya mfumo wa sasa wa sayansi na Teknolojia.
Katika kuipa sifa Skuli hiyo kongwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja
Balozi Seif aliwahimiza Wafaunzi wa Skuli hiyo kuwa na dhamira ya
kutafuta elimu kwa gharama yoyote ile.
Alisema wanafunzi lazima wawe na nia ya kutafuta elimu hasa ile ya
sayansi ambayo bado ina mapungufu katika taasisi za kijamii kwani
kuamua kusoma ni wajibu kwao ili kufanikiwa kimaisha.
Alifahamisha kwamba masomo ya sayansi yanayoonekana kupigwa chenga na
wanafunzi walio wengi maskulini ndio yanayotoa fursa kubwa ya ajira
katika ulimwengu huu wa sasa wa Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.
Skuli ya Kinyasini ikiwa ni miongoni mwa skuli kongwe ndani ya Mkoa wa
Kaskazini Unguja iliasisiwa mnamo mwaka 1946 kwa Darasa la Quran na
kuanza kwa darasa la kwanza mwaka 1947 lililoendelea hadi darasa la
kumi na moja Mwaka 1973 na sasa limefikia darasa na Kumi na Mbili.
No comments:
Post a Comment