Serikali imepanga kufanya mabadiliko ya kanuni za matumizi ya nyavu upande wa bahari ili wavuvi waweze kutumia nyavu za milimita nane badala ya milimita kumi zilizokuwa zikitumika awali.
Hayo yamesemwa leo, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi lililohoji kuwa ni lini Serikali itakuwa tayari kufanya utafiti katika eneo la Ziwa Victoria kama inavyofanya upande wa Bahari ili kuweza kuruhusu matumizi ya nyavu za chini ya milimita nane.
Ulega amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria, nyavu za kuvulia dagaa zenye ukubwa wa macho chini ya milimita nane zimekatazwa kutumika kwa uvuvi wa dagaa katika maji baridi ikiwemo maeneo ya maziwa kwa sababu tafiti zinaonyesha kuwa aina hiyo ya nyavu ikitumika itavua dagaa wachanga hivyo kuathiri uvuvi wa dagaa.
"Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania itafanya utafiti na endapo itaridhika itaruhusu wavuvi wanaovua ziwani wavue kwa kutumia aina hiyo ya nyavu, kwa upande wa bahari Serikali imeielekeza TAFIRI kufanya utafiti na kujiridhisha kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kanuni kwa haraka ili ikiwezekana tuweze kutumia nyavu za milimita nane zitakazoweza kuwanufaisha wavuvi wa upande wa bahari", alisema Ulega.
Amefafanua kuwa kwa upande wa bahari, nyavu zilizokuwa zikitumika kuvua dagaa ni milimita kumi lakini maoni ya wadau wengi yanaonesha kuwa milimita kumi zimeshindwa kuvua dagaa ndio maana Serikali imeamua kufanya utafiti huo ili kuona kama inawezekana wavuvi wa bahari kutumia nyavu za milimita nane.
Akizungumzia kuhusu uvuvi wa samaki aina ya Gogogo, Ngele na Mingu waliopo katika Ziwa Victoria, Naibu Waziri Ulega amesema kuwa katika mabadiliko ya Kanuni yanayofanyika hivi sasa Serikali imezingatia kufanya makubaliano ya kupitisha kanuni rasmi itakayoruhusu uvuaji na matumizi ya aina hizo za samaki.
Waziri Ulega ametoa rai kwa wavuvi kuendelea kuzingatia sheria na kanuni zilizopo kwani Sheria na kanuni hizo zinalenga uvuvi unaofanyika nchi uwe endelevu na wenye tija.
No comments:
Post a Comment