Rais na Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikuu cha UNISEL, Prof. Dkt. Mohammad Redzuan Bin Othaman akimkabidhi barua yenye kuainisha ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa Watanzania kwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhani Dau.
Dkt. Dau akiangalia miundombinu ya Chuo Kikuu cha UNISEL
Dkt. Dau akipata maelezo kuhusu uendeshaji wa chuo hicho.
Wageni kutoka Malaysia, Indonesia, Thailand na Ufilipino walipowasili Tanzania kwa ajili ya ziara ya mafunzo kwenye vivutio vya utalii.
Wageni kutoka Malaysia, Indonesia, Thailand na Ufilipino wakipata chakula.
Balloon lililowabeba wageni kuwazungusha katika mbuga ya Serengeti.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Vivutio vya Utalii kutangazwa Malaysia, Ufilipino, Thailand na Indonesia
Dodoma, 11 Aprili 2019
Makampuni 20 ya Mawakala wa Utalii na Tiketi za ndege (Tour Operators & Travel Agents) pamoja na Waandishi wa Habari kutoka katika nchi za Malaysia, Indonesia, Ufilipino na Thailand walifanya ziara ya mafunzo ya kutembelea vivutio vya utalii nchini kuanzia tarehe 1 – 7 Aprili 2019.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) yalijumuisha washiriki 20 ambapo Malaysia ilitoa washiriki 5, Thailand washiriki 6, Philippines Washiriki 4 na Indonesia washiriki 5.
Washiriki hao walitembelea maeneo mbalimbali yakiwemo Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mbuga ya Serengeti, duka Maarufu la kuuza madini ya Tanzanite, duka maarufu la zawadi la Arusha Cultural Heritage, sehemu ya historia ya masalia ya Binadamu wa Kale la Olduvai (Oldupai) Gorge na Kijiji cha Wamasai ili kujifunza uhalisia wa maisha yao. Wakiwa kwenye maeneo hayo, wageni walifanikiwa kuona wanyama maarufu watano- big five (Simba, Nyati, Faru, Chui na Tembo) na kushuhudia makundi ya Wanyama aina ya Nyumbu, Pundamilia, na Swala ambao hufanya ziara ya mzunguko maarufu kama Great Migration.
Wageni kabla ya kuagwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo pamoja na Bibi. Devotha Mdachi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii waliahidi kuitangaza Tanzania kama eneo jipya la utalii kwa nchi zao.
Wakati huo huo, Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhani Dau amepokea nafasi 160 za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu (scholarships) kwenye taaluma mbalimbali zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.9 sawa na Shilingi bilioni 4 za Tanzania. Ufadhili huo umetolewa na Chuo Kikuu cha Selangor (University of Selangor) ambacho pia kinajulikana kama UNISEL kilichopo katika Mkoa wa Selangor, Malaysia, unahusisha masomo ya Bachelors of Civil Engineering, Bachelors of Electrical Engineering, Bachelors of Mechanical Engineering, Bachelors of Occupational Health and Safety, Bachelors of Medical Laboratory, Bachelors of Industrial Biotechnology, Bachelors of Computer Science na Bachelors of Information Technology. Hivi karibuni Watanzania watafahamishwa utaratibu wa kuomba masomo hayo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
No comments:
Post a Comment