Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Ritta Kabati Gerald Malekela akitoa maelezo kwa viongozi wa timu shiriki kwenye mashindano ya Ritta Kabati Challenge Cup msimu wa tatu 2019
Baadhi ya viongozi wa timu shiriki kwenye mashindano ya Ritta Kabati Challenge Cup msimu wa tatu 2019 wakiwa makini kusikiliza maelezo kutoka kwa mwenyekiti wa mashindano.
NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
Jumla ya timu thelethini na sita (36) za mkoani Iringa kushiriki mashindano ya Ritta Kabati Challenge awamu ya tatu 2019 katika viwanja mbalimbali ya mpira wa miguu mkoani Iringa ambapo mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa siku ya jumamosi tarehe 15 / 06 / 2019.
Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Ritta Kabati Gerald Malekela amesema kuwa timu zilizoshiriki mashindano hayo zinatoka katika wilaya ya Mufindi,Kilolo na Iringa hivyo inajumuisha wilaya zote za mkoa wa Iringa.
“Kwa mara ya kwanza tumepata timu nyingi kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Iringa vijijini kwa kujitokeza timu kumi na moja hiyo inaonyesha jinsi gani kila kukicha mashindano haya yanazidi kuwa na mvuto na ushindani unaongezeka” alisema Malekela
Malekela alisema msimu huu mashindano yatakuwa bora kuliko misimu iliyopita kwa kuwa kamati imejipanga kuhakikisha wanatengeneza kitu kilicho bora na kuongeza thamani ya mashindano na kuweka alama ya kuigwa kwa wapenda michezo hasa mchezo huu wa mpira wa miguu.
“Tumejipanga kwelikweli kuhakikisha kuwa mashinda haya yanakuwa ya kiwango cha hali ya juu kiasi kwamba kila mtu atakuwa anavutiwa na mfumo wetu ambao tumekuwa tunautumia kuendesha mashindano haya” alisema Malekela
Malekela alisema kuwa lengo la mashindano hayo ni kukuza na kuibua vipaji vya wachezaji kutoka ngazi ya chini hadi kwenda kucheza ligi ambazo ni rasmi kama vile ligi daraja la kwanza la pili pamoja na ligi kuu katika nchi mbalimbali.
“Mwaka jana tulifaulu kwa kuhakikisha kuwa vijana wengi waliocheza mashinda haya walisajiliwa kwenye vilabu mbalimbli kuanzia ligi kuu hadi madalaja ya chini hivyo hayo nayo yalikuwa mafanikio makubwa kwetu” alisema Malekela
Aidha Malekela alisema kuwa mashindano hayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya ubovu na uhaba wa viwanja vya mpira wa miguu,hivyo tunaiomba serikali kuhakikisha wanatusaidia kuboresha viwanja hivyo
No comments:
Post a Comment