ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 7, 2019

UKEREWE: Upanuzi Kituo cha afya Bwisya kisiwani Ukara wafikia asilimia 95

Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella akiangalia ramani ya upanuzi wa Kituo cha Afya Bwisya kilichopo katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella leo Ijumaa Juni 07, 2019 amekagua maendeleo ya upanuzi na ujenzi wa Kituo cha Afya Bwisya kilichopo wilayani Ukerewe na kulidhishwa na ujenzi wake ambao umefikia asilimia 95 kwa mujibu wa mkandarasi.

Upanuzi wa Kituo hicho kwa hadhi ya Hospitali ni sehemu ya agizo la Rais Dkt. John Pombe Maguli alilolitoa baada ya ajali ya Kivuko cha MV. Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 ambapo alielekeza sehemu ya fedha za rambirambi ya ajali hiyo (Milioni 800) zitumike kufanya shughuli hiyo.

Mongella amesema ukarabati huo ulipaswa kukamilika mwezi Machi mwaka huu lakini umechelewa kutokana na changamoto ya miundombinu ya usafiri kwani baadhi ya vifaa ujenzi vinatoka jijini Mwanza na kusafirisha kwa njia ya maji hivyo matarajioni ni mkandarasi kampuni ya Suma JKT kukamilisha kazi hiyo mwishoni mwa mwezi huu.

Pia amekagua maendeleo ya Shule ya Sekondari Nyamanga iliyopo kisiwani Ukara aliyoiwekea jiwe la msingi la ujenzi Mei 02, 2019 na kuelekeza maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya madarasa kukamilika kwa wakati ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza walioanza masomo shuleni hapo kuelendelea vyema na masomo yao.

Aidha Mongella amekagua matayarisho ya ujenzi wa uzio, mnara na makaburi ya baadhi ya abiria wa Kivuko cha MV. Nyerere waliozikwa katika malalo ya pamoja eneo la Bwisya kisiwani Ukara na kuelekeza Suma JKT kukamilisha pia shughuli hiyo kwa wakati.


Itakumbukwa kwamba Novemba 17, 2018 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo alizindua rasmi ujenzi wa miundombinu katika Kituo hicho unaofanywa na kampuni ya SUMA JKT chini ya usimamizi wa Kamati Maalum iliyoundwa na Mongella.
Kukamilika kwa upanuzi wa Kituo cha Afya Bwisya, kutaondoa adha kwa wananchi zaidi ya elfu thelathini waliokuwa wakivuka maji kwenda Mjini Ukerewe ama Jijini Mwanza kufuata huduma za afya.

Sehemu ya majengo yaliyojengwa kwenye Kituo cha Afya Bwisya wilayani Ukara. 
Tenki la kuhifadhia maji katika Kituio cha Afya Bwisya.
Majengo yaliyojengwa kwenye Kituo cha Afya Bwisya ni pamoja na nyumba ya mtumishi, maabara, wodi ya wazazi, jengo la upasuaji na jengo la kuhifahia maiti.
Upanuzi wa Kituo cha Afya Bwisya umefikia asilimia 95 ambapo asilimia tano zilizosalia zinatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 17, 2019.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella akikagua maendeleo ya upanuzi wa Kituo cha Afya Bwisya kilichopo Ukara wilayani Ukerewe.
Sehemu ya madarasa katika Shule ya Sekondari Nyamaga kisiwani Ukara.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hii Mei 02, 2019 na kufufua ujenzi wake ambao ulikuwa unasua sua tangu mwaka 2014.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella pamoja akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali amekagua matayarisho ya ujenzi wa mnara, uzio na makaburi ya baadhi ya abiria waliofariki kwenye ajali ya MV. Nyerere na kuzikwa katika eneo la Bwisya kisiwani Ukara.
Baadhi ya viongozi wa CCM wilayani Ukerewe wakiwaombea ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza majisha kwenye ajali ya Kivuko cha MV. Nyerere kilichokuwa kikitoka Kisiwa cha Bugolora kwenda Kisiwa cha Bwisya.
TAZAMA>>> RC Mongella akagua ujenzi wa Hospitali ya Bwisya wilayani Ukerewe

No comments: