LICHA ya aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa Tanzania, Emmanuel Amunike kutimuliwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, inadaiwa kocha huyo bado yupo nchini akisubiri kulipwa malimbikizo ya mshahara wake.
Amunike alitemeshwa kibarua cha kuifundisha Stars, Julai 8 baada ya kupata matokeo mabovu katika fainali za Afcon zilizofanyika nchini Misri.
Mwanaspoti linafahamu kocha huyo anadai mishahara ya miezi minne, hali ambayo inamfanya aendelee kuzunguka mjini akisikilizia pesa zake.
Chanzo kimoja cha ndani ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kililiambia Mwanaspoti kuwa, kocha huyo alitakiwa apewe pesa zake tangu Julai 22, lakini umeendelea ukimya ambao umemfanya abaki nchini.
“Kocha alitakiwa awe ameshaondoka, lakini kumekuwa na ukimya juu ya pesa zake, tunaamini kila kitu kitakuwa sawa hivi karibuni,” kilisema chanzo hicho.
Awali, Amunike alikuwa anakaa katika hoteli ya White Sands, lakini hivi sasa amehamishia makazi yake maeneo Oysterbay.
Mwanaspoti lilimtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao ili kufafanua suala hilo na kukiri kuwa ni kweli kocha huyo bado yupo nchini akisubiri pesa zake, lakini atapewa kutokana na wao pia kuwa wanasubiri mgawo kutoka Shirikisho la soka duniani (Fifa).
“Kweli anatudai pesa zake lakini tayari za kwanza kutoka Fifa ziliwekwa Januari, tunasubiri zingine ambazo zitaingia mwanzoni mwa Agosti na ndipo tutamlipa na kumalizana naye,” alisema Kidao.
No comments:
Post a Comment