Muonekano wa Shamba la Serikali la Makuwe liliopo Mkoa wa Kaskazini Pemba ambalo Mwaka 2017 limekodishwa Mikarafuu yake kwa gharama ya shilingi Milioni 290,000,000/-.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea na kukagua Mashamba ya Serikali yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Kisiwani Pemba Nd. Said Juma Hamad Kushoto akitoa maelezo ya mazingira yaliyopo ya Mashamba ya Serikali Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Baadhi ya Wananchi na Wakulima wa Vijiji vya Finya na Makuwe waliojitokeza kumlaki Balozi Seif aliyefika katika Vijiji hivyo kukagua Mashamba ya Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa maagizo ya utafutwaji wa Mashamba ya Serikali wakati alipofanya ziara ya kuyakagua Mashamba ya Serikali ya Finya na Makuwe Kisiwani Pemba.
Naibu Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za
Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Shamata Shaame
Khamis akitoa ushauri wa namna ya kusafishwa Mashamba ya Serikali kwa
kutumia Vikosi vya SMZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa maamuzi mara baada ya
kukamilisha zoezi la uhakiki wa Mashamba yake yote yaliyomo katika
maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
Alisema maamuzi hayo pamoja na mambo mengine yatazingatia pia kuwapa
Wananchi ili wayaendeleze kwa kilimo hasa yale yaliyokosa usimamizi na
kuyaendeleza kwa muda mrefu na kusababisha uzalishaji mdogo wa mazao
pamoja na Karafuu.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiendelea na ziara yake ya
Siku Nne Kisiwani Pemba akikagua Mashamba yanayomilikiwa na Serikali
yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema umefika wakati Mashamba ya Serikali yawe na uwezo kamili wa
uzalishaji kama yalivyo ya Watu Binafsi na pale inaposhindikana kukosa
huduma za usafishaji ni vyema ukaandaliwa utaratibu na Taasisi
zinazohusika kuwapa Wananchi wale wenye nia ya kuyaendeleza kwa
Kilimo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iko tayari kuridhia Wizara ya Kilimo , Maliasili, Mifugo na
Uvuvi Zanzibar kuandaa utaratibu wa kutoa Ajira kwa Vijana ili
yasafishwe Mashamba yote ya Serikali ambayo hukaa muda mrefu na
kupoteza Uzalishaji.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mbali ya usafishaji wa Mashamba hayo
utakaoongeza Mapato ya Taifa lakini kwa upande mwengine fursa hiyo
itatoa ajira kwa Vijana watakaokuwa tayari kufanya kazi hiyo ya
Kizalendo ya kuokoa Uchumi wa Taifa.
Aliushauri Uongozi wa Wizara ya Kilimo mbali ya kufanya Uhakikishi
utakaoongozwa na Wakuu wa Wilaya wa kuyatambua Mashamba ya Serikali
katika Wilaya mbali mbali lakini wakazingatia kuwahakiki Wananchi
waliyojitolea kuyasafisha Baadhi ya Mashamba hayo bila ya
kushurutishwa.
Alisema uhakiki huo uwaandalie Wanachi hao njia na namna ya kuandika
Maombi na kuyapeleka Serikalini kupitia kwa Masheha na Wilaya zao
yatakayotoa utaratibu wa kumilikishwa katika matumizi yake kama
ilivyofanywa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume Mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Akitoa ushauri wa kunawirishwa kwa Mashamba ya Serikali, Naibu Waziri
wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara
Maalum za SMZ Mh. Shamata Shaame Khamis alisema ni vyema vikatumiwa
Vikosi vya SMZ wakiwemo Watu wa Chuo cha Mafunzo katika usafishaji wa
Mashamba hayo.
Mh. Shamata alisema hatua hiyo ya dharura inaweza kusaidia kipindi
hichi cha mpito kuelekea mafuno ya Msimu wa Vuli ambao hutegemea
kuzalisha mazao mengi haza lile la Uchumi wa Taifa la Karafuu.
Alisema Vikosi cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na mambo
mengine ya Ulinzi lakini pia vina utaratibu wa kushiriki kwenye
shughuli za Kijamii na Kitaifa pale inapotokeza kuwepo kwa mahitaji
hayo.
Mapema Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Kisiwani Pemba
Nd. Said Juma Hamad alisema yapo Mashamba Sita yanayomilikiwa na
Serikali Kisiwani pemba ambayo hayako katika hali ya kuridhisha
kutokana na ushughulikiaji mdogo.
Nd. Said alitolea mfano Shamba la Makuwe pekee linalotegemewa na
Serikali kwa mapato Makubwa lenye ukubwa wa Ekari 200 likiwa na
Wafanyakazi Watano tu wanaolihudumia.
Alisema Shamba hilo lililosheheni zaidi miti ya Mikarafuu na Minazi
limefanyiwa usafi Mnamo Mwaka 2016 kukodishwa kwa zaidi ya Shilingi
Milioni 290,000,000/- katika kipindi cha Msimu wa Vuli mnamo Mwaka
uliofuatia wa 2017.
Mkuu huyo wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Pemba
alifahamisha kwamba Minazi iliyomo ndani ya Shamba la Makuwe nazi zake
hutumika kuoteshea Miche kwenye Vitalu vya Wizara ya Kilimo na baadhae
kugaiwa kwa Wakulima.
Naye Afisa Mdhamini wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar {ZSTC}
Kisiwani Pemba Ndugu Abdullah Ali Ussi alisema Shirika hilo
limefurahishwa na utaratibu uliobuniwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar wa kuyafuatilia kwa uhakiki na utambuzi Mashamba yake yote.
Nd. Abdullah alisema kutokana na kutoshughulikiwa kwa mashamba ya
Serikali ambayo ndio yenye uwezo wa kuzalisha zao la Karafuu kwa
wingi kumesababisha kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo katika Miaka ya
karibuni na kufika Tani 8,500 wakati miaka ya nyuma uzalishaji
ulifikia hadi Tani 16,000.
Akitoa ufafanuzi wa Mashamba ya Serikali Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi Bibi Maryam Abdallah Saadala alimueleza
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba njia pekee ya kuyaokoa
Mashamba ya Serikali na kupatikana ajira za Muda kwa Watu
watakaosafisha Mashamba hao.
Bibi Maryam alisema Mashamba Sita yaliyopo Kisiwa cha Pemba yanaweza
kuwa katika mazingira bora iwapo Serikali kupitia Taasisi inayosimamia
Utumishi wa Umma itaridhia kutoa baraka za upatikanaji wa Vijana
watakaoajiriwa kwa muda kufanya kazi hiyo muhimu.
Alisema mfumo huu unaweza kutumika kwa muda pale inapotokea dharura
ya kutaka kusafishwa Mashamba hayo hasa ule wakati unaofuatia baada ya
Msimu wa Mvua Kubwa hapa Nchini.
Akiambatana na baadhi ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Watendaji Wakuu
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alipata wasaa wa kuyakagua Mashamba ya Serikali yaliyo chini
ya Wizara ya Kilimo, Maliasilini. Mifdugo ya Uvuvi yaliyopo katika
Vijiji vya Finya na Makuwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
No comments:
Post a Comment