Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi (hawapo pichani),katika Kijiji cha Society wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi kabla ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi Kijiji cha Ntibiri wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi wakati alipofika kukagua kazi ya usambazaji umeme kwenye Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kushoto) akikata utepe kuashiria uwashaji umeme katika Kijiji cha Kirida wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi.
Na Hafsa Omar, Katavi
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa vyombo vya usalama mkoani Katavi kuwakamata wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme vijijini mkoani humo kutoka kampuni ya CRCBEG baada ya kusuasua katika utekelezaji wa kazi.
Alitoa agizo hilo Agosti 25, 2019 wakati akielekea kwenye kijiji cha Ntibiri wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi ili kukagua kazi ya usambazaji umeme, mara baada ya kuwasha umeme katika kijiji Kirida wilayani humo.
Waziri wa Nishati pia alitoa agizo la kushikiliwa kwa hati za kusafiria za wakandarasi hao mpaka watakapomaliza kazi zao za usambazaji umeme walizopangiwa na Serikali.
“ Nilitoa mwezi mmoja eneo lote la kilometa 27 muwe mmeshawasha umeme lakini bado, Kijiji cha Majimoto bado hamjawasha, leo nimepita hapa sijaona vibarua wakihangaika, na wala nguzo hazijafika, nimefika Shule ya Sekondari kule nguzo hazijafika na wala hamjasambaza popote.”alisema Dkt. Kalemani.
Waziri Kalemani, pia aliwaagiza Mameneja wa TANESCO kutoondoka katika eneo hilo ili kuhakikisha kazi ya usambazaji umeme inafanyika kwa kasi zaidi, “ninataka umeme ufike Kijiji cha Majimoto, ifikapo tarehe 5 mwezi ujao na mameneja wote mtabaki hapa kusimamia kazi.”
Akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Ntibiri, Dkt. Kalemani aliwaeleza wananchi hao kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 89 kwa ajili ya usambazaji umeme mkoani Katavi na kuwahakikishia kuwa, mkoa mzima utapata umeme.
“Leo nimetoa maelekezo kuwa, eneo la Ntibiri na maeneo ya jirani, wakandarasi watamaliza kazi mwezi wa 12 mwaka huu, hakuna kijiji kitakachobaki, sasa kama eneo lako halijapitiwa na umeme, kuanzia sasa litapitiwa.” Alisema Dkt Kalemani
Akiwa wilayani Mlele, Waziri wa Nishati, pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Society katika eneo la wachimbaji wadogo wa dhahabu hali itakayopelekea wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa tija.
No comments:
Post a Comment