ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 26, 2019

KUTAFUTA MFANYAKAZI WA NDANI MARUFUKU TARAFA YA ITISO - AFISA TARAFA ITISO

 Afisa Tarafa Itiso Bw.Remidius Emmanuel akihutubia wananchi waliojitokeza katika Mahafali ya Darasa la saba Shule ya  msingi Zajilwa.
AfisaTarafa Itiso Bw.Remidius Emmanuel akipata maelezo ya jambo flani kutoka kwa mkuu wa shule hiyo Bw. Joseph Nicholaus Lusambo katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Zajilwa.
 Risala ya Mkuu wa shule kwa Mgeni rasmi ikikabidhiwa na Mwalimu Fatuma Abubakari katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Zajilwa.
 Diwani wa Kata ya Zajilwa Mhe.Farida Ramadhani akizungumza na wananchi waliojitojeza katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Zajilwa.



 Baadhi ya Wananchi waliohudhuria katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Zajilwa

Picha na baadhi ya wahitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Zajilwa.


AFISA Tarafa Itiso Remidius Emmanuel amesema kuwa tarafa hiyo siyo sehemu kutafuta wafanyakazi wa ndani hasa katika nyakati hizi ambazo wanafunzi wa darasa la saba wanahitimu masomo yao.

Akizungumza katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Zajilwa Afisa tarafa wa Itiso Remidius Emmanuel ameonekana kukerwa na  baadhi ya watu ambao wameendelea kuwekeza kwa wahitimu wa darasa la saba  kwa lengo la  kuwaandaa wakawe wafanyakazi wa ndani "House Girl".

"Nimewatazama wanafunzi wakati wote wakiimba hapa na kuagana na wenzao, nimesikiliza pia risala yao, lakini nilipouliza wangapi wanayo matumaini ya kufaulu wote wamenyoosha mikono, tafsiri yake ni kwamba wanayo ndoto ya kusonga mbele, sasa huwa ninakerwa sana na ile dhana ya watu kutoka maeneo mbalimbali wanapiga simu kutafutiwa wafanyakazi ndani ya tarafa yetu Itiso, wakiwambia muwatafutie wafanyakazi wa ndani wambieni Tarafa ya Itiso sio mahala pake, hatuwaandai kuwa wafanyakazi wa ndani bali tunahitaji wafaulu na kuendelea na elimu ya Sekondari na siku za usoni kupitia kwenu tupate wataalamu katika fani mbalimbali ili waendelee kulijenga taifa" Ameeleza.

Na amewaonya wazazi ambao kwa namna moja au nyingine  watakuwa kikwazo kwa wanafunzi hao kuendelea na Elimu ya Sekondari ikiwa wamefaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo yao.
"Ninazo taarifa za baadhi ya wazazi kuwa kikwazo na kutamani watoto wao kufeli masomo yao, ole wao wabainike kuwa chanzo cha vijana hawa kutoendekea na masomo" Ameongeza.

Mapema akisoma risala mbele ya mgeni rasmi mkuu wa shule ya Msingi Zajilwa  yenye jumla ya  wanafunzi 1,239 Mwalimu Joseph Lusambo ameeleza kuwa jumla ya wanafunzi 84 wanatarajiwa kuhitimu elimu yao ya msingi katika shule hiyo kwa mwaka 2019 na kwamba wanayomatumaini makubwa juu ongezeko la ufaulu kwa mwaka huu ikilinganishwa na miaka iliyopita kutokana na maandalizi ambayo yamefanyika shuleni hapo huku akizitaja sababu za matarajio ya ufaulu kuongezeka kuwa ni pamoja na  uwepo wa ufaulu bora kwa mitihani ya kujipima sambamba na ubora na juhudi za walimu waliopo.

Mkuu wa shule hiyo amezitaja baadhi ya changamoto shuleni hapo kuwa  ni pamoja na ukosefu wa vitabu vya kutosha,vyumba vya Madarasa ambapo  vyumba vilivyopo ni 8 kati ya 27 vinavyohitajika, hatua inayopelekea baadhi ya wanafunzi kusomea nje.

Mbali na kuwahimiza wanafunzi wanaobaki shuleni hapo kuhakikisha wanasoma kwa bidii, Diwani wa kata ya Zajilwa Farida Ramadhani  amesema kuwa tayari  changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa imeanza kufanyiwa kazi kufuatia uwepo wa tofali 35,000 zitakazo saidia kufanikisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na tayari Serikali ya kijiji hicho  imepitisha  fedha kwa  ajili ya kuanza ujenzi wa awali na kinachosubiliwa  kuidhinishwa kwenye mkutano wa Wananchi na kushirikisha wataalam wa  Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa kila hatua.

Katika hatua nyingine Afisa Tarafa huyo alitambua na kupongeza juhudi zinazofanywa na Mbunge wa jimbo hilo la Chilonwa  Joel  Mwaka ambaye kwa nafasi yake amekuwa msaada mkubwa katika kufuatilia na kusimamia maendeleo ya shule hiyo.

Akihitimisha hotuba yake mbali na kuhimiza Wazazi,Walimu,Jamii pamoja  na wanafunzi kila mmoja kutimiza wajibu wake, Afisa tarafa huyo alisema kwa suala la upatikanaji wa Vitabu, Serikali inaendelea kutatua changamoto hiyo
 " ninazo taarifa kwamba  ndani ya kipindi hiki cha mwaka  huu 2019 takribani Vitabu 317  vimetolewa na Serikali katika shule hii, ingawa pamoja na juhudi za Serikali  bado upo umuhimu wa kushirikiana na wadau mbalimbali kuona namna ya kukabiliana na changamoto za namna hii na  jambo hilo  linawezekana" alieleza.

Mahafali hayo pia yalihudhuriwa na Afisa Elimu wa kata hiyo  Heri Justine Mhinda, Wataalamu kutoka ngazi ya kata na vijiji, Wajumbe wa Serikali ya kijiji, Viongozi wa dini pamoja na wananchi wa Kijiji hicho.


No comments: