Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake kutembelea miradi inayosimamiwa na DAWASA na kuzungumzia hatua mbalimbali ilipofikia na kuwaondoa hofu wakazi wa maeneo ya Mkuranga baada ya kukaa bila maji safi kwa kipindi kirefu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange akiangalia mafundi wa DAWASA wakiwa wanaunganisha mabomba kabla ya kuyalaza, ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ilikua sambamba na wajumbe pamoja Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja.
Msimamizi wa mradi wa maji Mkuranga kutoka DAWASA, Mhandisi John Kirecha akielezea ramani ya mradi wa Maji Mkuranga kuanzia kwenye chanzo cha maji Kulungu kuelekea kwenye tanki la maji la ujazo wa Lita Milioni 1.5 leo wakati wa ziara ya mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange pamoja na wajumbe wa bodi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange akiyajaribu maji kwa kuyaonja kutoka kwenye kisima kilichopo Mkuranga kitakachohudumia wakazi wa maeneo hayo.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange amewaondoa hofu wakazi wa Mkuranga na kuwataka kuwa na subira kwani kero ya maji inakaribia kumalizika.
Hayo ameyasema wakati wa ziara yake katika mradi wa maji wa Mkuranga ulioanza kutekelezwa hivi karibuni ukiwa umefikia kwenye hatua ya ujenzi wa tanki la maji na ulazaji wa mabomba.
Mwamunyange amesema, kulikuwa na changamoto zilijitokeza katika mradi huo ila kwa sasa zimeshapatiwa ufumbuzi na wakandarasi wameshaingia kazini.
“Napenda kusema hakuna udanganyifu katika mradi wa Mkuranga ila kulikuwa na changamoto zilijitokeza na kwa sasa zimeshapatiwa uchambuzi na wakandarasi wameingia kazini kuendelea na kazi,”amesema Mwamunyange.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huu ni moja kati ya miradi sita iliyosainiwa hivi karibuni ukiwa na thamani ya Bilion 5.5 na inatarajia kukamilika ndani ya miezi nane kuanzia sasa.
Luhemeja amesema, kukamilika kwa mradi huu utahudumia wananchi 25,000 ambapo maji yatasambazwa katika Vitongoji mbalimbali vya Wilaya ya Mkuranga.
“Katika mradi huu kutakuwa na ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa Lita Milion 1.5 ambapo litasambaza maji katika maeneo mbalimbali na zoezi la ulazaji wa mabomba linaendelea kwa sasa na wameangalia ubora wa mitaro kwa kuchimba urefu wa mita 1.5 na mabomba yote ni mapya.
"Hatutarajii kuona kuna changamoto ya upotevu wa maji katika mradi huu, kwani mabomba yote ni mapya pia tumeangalia ubora wa mitaro kwa kuchimba mita 1.5 kwenda chini na utakamailika ndani ya muda wa miezi nane tokea sasa,"amesema.
Msimamizi wa mradi huo kutoka DAWASA, Mhandisi John Kirecha ameweka wazi kuwa wameweza kufuata taratibu mbalimbali za kitaalamu kabla ya kuendelea na ujenzi ambapo walichukua sampo ya mchanga eneo la ujenzi wa tanki na kupeleka DIT na wakapata ushauri wa kuchimba urefu wa Mita 2.5 kwenda chini.
Pia, ameeleza kuwa watafunga Booster itakayosaidia kusafirisha maji kwa kasi kuelekea kwenye tanki la maji la Mwanambaya lenye ujazo wa Lita 100,000 litakalotumika kama tanki la akiba ( reserve).
Mradi wa Mkuranga unatarajiwa kukamilika mapema 2020, na utahudumia Mkuranga na vitongoji vyake, maeneo ya Viwanda Kisemvule, Vikindu na wananchi wa maeneo hayo wamefurahi kuja kwa mradi huo kutoka chanzo cha Maji Kulungu ambapo wamekaa na shauku ya kupata maji safi na salama kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment