ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 27, 2019

SERIKALI YAZINDUA UJENZI WA VIVUKO VIPYA VYA BUGOROLA-UKARA, CHATO-NKOME

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Eng. Japhet Maselle (wa tatu kushoto) akimuongoza Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Eng. Warioba Sanya (katikati), kwenda kuzindua ujenzi wa vivuko viwili vipya vya Bugorola-Ukara Wilaya ya Ukerewe na Chato nkome Wilaya ya Chato. Uzinduzi huo ulifanyika jana katika karakana ya Songoro Marine Boartyard Ltd iliyoko Ilemela, jijini Mwanza.
 Eng. Warioba Sanya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akizindua ujenzi wa kivuko kipya cha Chato-Nkome (wilaya ya Chato) kinachojengwa na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard Ltd ya jijini Mwanza, kwa gharama ya Tshs Bilioni 3.1 fedha inayotolewa na Serikali ya Tanzania. Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 yaani abiria 200, magari 10 na mizigo. Ujenzi wa kivuko hiki utakamilika ndani ya Wiki 40.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Eng. Japhet Maselle (kushoto) akimpongeza Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Eng. Warioba Sanya (kulia) baada ya kukamilisha uzinduzi wa ujenzi wa vivuko vipya viwili kwa ajili ya maeneo ya Chato-Nkome (Chato) na Bugorora-Ukara (Wilaya ya Ukara) Mkoa wa Mwanza. Uzinduzi huo ulifanyika jana katika karakana ya Songoro Marine Boatyard Ltd, Ilemela jijini Mwanza. 

SERIKALI imezindua rasmi ujenzi wa vivuko vipya viwili vya kisasa vitakavyotoa huduma ya kusafirisha abiria, mizigo na magari kati ya Bugorola-Ukara Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza na Chato-Nkome Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Uzinduzi wa ujenzi huo umefanyika jana mkoani Mwanza katika eneo la karakana ya Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard Ltd, inayojenga vivuko hivyo ambapo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe pamoja na taasisi mbali mbali zilizo  chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Maselle alisema Serikali imeamua kujenga vivuko hivyo kutokana na kuwapo kwa uhitaji mkubwa wa huduma ya vivuko kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mhandisi Maselle alisema kivuko cha Bugorola-Ukara kinajengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard Ltd kwa gharama ya Tsh bilioni 4.2 na kile cha Chato- Nkome kinagharimu Tsh bilioni 3.1

“Vivuko vyote vinagharimu jumla ya Tsh bilioni 7.3 fedha zinazotolewa na Serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi mahiri wa Jemedari, Rais wetu, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, na kwa mujibu wa mikataba tuliyoingia na kampuni hii ni kwamba vivuko hivi vitajengwa kwa miezi 10, hata hivyo namuagiza mzabuni akamilishe ujenzi wa vivuko hivi kwa chini ya muda huo”.

Kivuko cha Bugorola-Ukara kitakuwa na na vipimo vya urefu wa mita 39, upana mita 10 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0-7 hadi 1.0, pia kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 yaani abairia 300, magari 10 na mizigo, vile vile kivuko cha Chato-Nkome kitakuwa kitakuwa na vipimo vya urefu wa mita 37, upana mita 10 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0-7 hadi 1.0, pia kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 yaani abairia 200, magari 10 na mizigo.

Vivuko hivi vitafungwa injini mbili kila kimoja, HP 350 kwa kivuko cha Bugorola-Ukara na HP 300 kwa kivuko cha Chato-Nkome na vitaendeshwa na mifumo miwili ya usukani ambapo mmoja utakuwa ni wa dharura. Lengo la serikali ni kuimarisha usalama majini na usafiri wa uhakika ndio maana vivuko hivi vinajengwa kwa mabati maalum ya daraja la kwanza ‘grade A marine’ 

Naye Mkurugenzi  Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard  Ltd, Major Songoro aliipongeza Serikali kwa kuiamini kampuni yake na kuipatia zabuni za kujenga vivuko hivyo huku akiahidi kuvikabidhi mapema mwezi Februari badala ya Aprili kama ilivyo kwenye mkataba. 

Kwa upande wa Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Warioba Sanya alisema ujenzi wa vivuko hivyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya kutaka kuboresha   na kuimarisha usalama wa abiria na vyombo vya majini ndani ya Ziwa Victoria.
“Hapa kinachotekelezwa ni ahadi ya rais wetu na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatutaki yale yalitokea Bugorola yatokee tena, sote tunajua mahitaji yaliyopo pale Bugorola ingawa kuna kivuko cha MV Sabasaba kinafanya kazi pale”.

Aliongeza kuwa Serikali imekusudia kuwawezesha wakandarasi wa ndani ili kusudi kodi za watanzania ziweze kubaki hapa nchini kwa watanzania wenyewe. Mkoa wa Mwanza sasa upo katika mkakati maalumu wa kuwa kituo cha uchumi katika nchi za Afrika Mashariki, ndio maana tunataka kampuni hii iwezeshwe na kuwa mahiri ili iweze kujenga meli kubwa hapa hapa jijini Mwanza. Hivyo nawaagiza viongozi wa kampuni hii kujenga vivuko hivi kwa ufanisi na kasi kubwa.

No comments: