ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, August 21, 2019
Shahidi kesi ya akina Mbowe adai uwanja wa mkutano haukuwa na alama za utambuzi
By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Shahidi wa sita katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amedai eneo la mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni za Chadema halikuwa na utambuzi wa alama.
Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam Kisutu, Tanzania.
Shahidi huyo ambaye ni askari polisi mwenye namba F 5392 Koplo Charles (40, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Agosti 21, 2019 wakati akihojiwa na upande wa mashtaka.
Ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kuulizwa swali na wakili wa Serikali, Jaqline Nyantori kwa nini katika video iliyoonyeshwa mahakamani hapo haikuonyesha jina la viwanja vya Buibui vilivyopo Mwananyamala ulikofanyika mkutano huo.
Akijibu swali hiyo, shahidi huyo amedai eneo hilo halikuwa na kibao kinachoonyesha viwanja hivyo ni vya Buibui.
"Hakukuwa na kibao wala alama ya utambuzi, na mimi nilikwenda pale kwa ajili ya kuchukua matukio ya mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chadema,” amedai.
Habari zinazohusiana na hii
Shahidi huyo amedai kuwa dio alipangwa na ofisi yake kwenda kuripoti na kupiga picha katika mkutano huo wa Chadema wa kufunga kampeni.
Amedai Februari 16,2018 asubuhi aliingia kazini kama kawaida na kuhudhuria kikao cha kazi ambacho hufanyika kila siku ofisi hapo kikiongozwa na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa wa kipolisi Kinondoni,SSP John Malulu.
"Katika kikao hicho cha asubuhi mada kubwa ilikuwa ni kuhusiana na ufungaji wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni,” amedai shahidi huyo ambaye aliyeajiriwa na Jeshi la Polisi tangu mwaka 2003.
“Niliambiwa na SSP Malulu kuwa ikifika saa 10:00 jioni ya Februari 16, 2018 niende nikachukue matukio ya mkutano wa Chadema wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni.”
Amebainisha kuwa baada ya kupewa maelekezo hayo, alijiandaa kwa kuangalia kamera yake kama ina chaji ya kutosha na ilipofika saa 9:30 alasiri alienda katika mkutano huo.
Amedai baada ya kufika alikuta maandalizi yakiendelea na watu wakiendelea kukusanyika katika eneo hilo.
Baada ya shahidi huyo kumaliza kuhojiwa na upande wa mashtaka, hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo kwa muda.
Kesi hiyo itaendelea tena baadaye kwa shahidi wa saba upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa wao.
Tayari mashahidi sita wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao akiwemo, Daktari kutoka Hospitali Kuu ya Jeshi la Polisi, Kilwa Road.
Katika ushahidi wake Dk Juma Khalfani (54) alieleza askari waliojeruhiwa katika maandamano ya Chadema, walipigwa na kitu chenye ncha kali na butu.
Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu makatibu wakuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara); mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hichi, Dk Vicent Mashinji.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama ambapo wote wanadaiwa kuwa Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment