DENI la shilingi milioni tano kati ya Shilingi 5,364, 814.2 ambalo Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kulipa ikiwa ni gharama za matibabu ya marehemu Bi. Sabina Kitwae Loita, leo limelipwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako Bi. Sabina alikuwa akipatiwa matibabu.
Fedha hizo ambazo zimechangwa na wananchi zimewasilishwa MNH na wakili Albert Msando kwa niaba ya wananchi hao.
Bi. Laila Kitwae ambaye ni mtoto wa marehemu Sabina Kitwae Loita alitoa ombi la kusaidiwa gharama za matibabu ili aweze kuchukua mwili wa marehemu mama yake Agosti 11 mwaka huu wakati Rais Magufuli alipotembelea Muhimbili kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo alipokuwa akikabidhi fedha hizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru, wakili Msando amesema kuwa amelipa fedha hizo baada ya kuchangisha katika mtandao wa kijamii na amewataka wananchi kulipa gharama za matibabu kwa kuwa MNH ina mahitaji mengi katika kujiendesha.
“Mimi binafsi kupitia akaunti yangu ya Instagram nilihamasisha wananchi ili tuweze kulipa hili deni. Kwanza sababu kuu ya kufanya hivyo ni kuwahamasisha kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, pili Mheshimiwa Rais ni binadamu kama nilivyo mimi na wewe ambaye naye anaguswa kama ambavyo aliguswa na tatizo hili na kuahidi kulipa deni hili.
“Tatu, wananchi wafahamu kuwa hospitali kubwa kama Muhimbili ina mahitaji mengi, hivyo wanatakiwa kuchangia huduma za matibabu,” amesema Msando.
Akipokea kiasi hicho cha fedha Museru amewashauri wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili waweze kusaidiwa kupata matibabu mara wanapohitaji huduma.
“Gharama za matibabu ni ghali, tunapoboresha huduma za matibabu gharama ya kutoa tiba zinazidi kuongezeka. Kwa mfano kutakuwa na CT-Scan, MRI na kutakuwa na gharama za uchunguzi wa maabara, zote hizi ni gharama na kwa kawaida zinaongezeka hivyo Watanzania wanapaswa kuchangia huduma ili fedha zinazopatikana zitumike kutoa huduma,” amesema Prof. Museru.
Na: Sophia Mtakasimba GPL
No comments:
Post a Comment