KAMA ni kiu ya kupata mtoto kwa sasa mwigizaji nyota wa filamu Bongo, Wema Isaac Sepetu amefika kisimani; kinachosubiriwa ni kuteka maji na kuyanywa; Gazeti la Ijumaa Wikienda limethibitishiwa.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Wema aliyesaka mtoto kwa miaka mingi bila mafanikio amesema, madaktari waliokuwa wakifuatilia afya yake ya uzazi wamemwambia; “Kila kitu kwenye tumbo lako la uzazi kimekaa sawa na sasa unaweza kuzaa bila tatizo lolote.”
WEMA AONDOA HOFU
Kutokana na majibu hayo ya kitabibu, Wema ambaye ni Miss Tanzania 2006, ameondoa hofu ya kutokuzaa aliyokuwa nayo mwanzo na kusema sasa yuko tayari kuitwa mama. “Mwanzo nilisema nikifika umri wa miaka 30 kama sijapata mtoto, itanilazimu kufunga kizazi, lakini madaktari wameniambia ninaweza kupata ujauzito kuanzia Januari, mwaka ujao.
“Awali waliniambia siwezi kupata mtoto kwa sababu mfuko wa kizazi ulikuwa umejaa mafuta pia kulikuwa na vitundu ambavyo vilisababisha mbegu za uzazi zishindwe kupevuka,” alisema Wema muda mfupi kabla ya kulazwa kwenye hospitali moja jijini Dar akisumbuliwa na presha.
Kutokana na Wema kukosa mtoto kwa miaka mingi, baadhi ya watu hasa mahasimu wake wamekuwa akimkejeli kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa ni mgumba, jambo ambalo limekuwa likimhuzunisha mara kadhaa na yeye kuwajibu watu hao kwa maneno mazito;
“Mnadhani ninaipenda hii hali… Hata mimi natamani kuitwa mama na hakuna kinachoniuma kama hicho….So mnadhani sijui kama umri unakwenda na maisha yenyewe siku hizi mafupi, any time we die…Mnafikiria nisingependa kuacha hata kacopy kangu siku ndo’ Mungu anasema ananichukua?
“Hata mimi natamani ningekuwa napiga picha niko na mwanangu… I want dat with all my life but I cant…. Sitakaa nimkufuru Mungu wangu hata siku moja maana sijui ni kitu gani kaniandikia,” aliandika haya Aprili 12, 2015 kwenye mtandao wake wa Instagram.
“Binafsi ninawapenda sana watoto, hivyo ninajihisi kuwa huru kuposti picha zao, lakini mashabiki hawanielewi, huwa wananiita mgumba, tasa na maneno kama hayo ya kuniudhi.
“Wakati mwingine wananitumia ujumbe na kuniambia; “Zaa wa kwako”, au “Utaishia kuposti picha za watoto wa wenzako.”
“Binafsi huwa ninaumia sana, kwa kuwa sina moyo wa chuma,” kauli hii aliitoa Juni, 2016 alipofanya mahojiano na gazeti moja la michezo nchini.
SASA ATAMANI MTOTO WA KIUME
Baada ya kuhakikishiwa mwanga wa kupata ujauzito mapema mwakani, Wema ameonesha kiu yake kwa kusema; “Napenda mtoto wangu wa kwanza awe wa kiume.
“Wa kwanza akiwa wa kiume ataweza kuwaongoza wenzake watakaofuata, lakini kama Mungu hakupenda hilo hata wa kike si mbaya.”
BABA KIJACHO ANAYE?
Uzazi kwa binadamu hauji kwa tunguli za kiganga kuna prosesi zake ambapo Wema alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu baba kijacho yupo au ndiyo anamsaka? Alisema; “Yupo. Ila watu wavumilie tu kwa sasa, sitaweza kumuweka wazi, siku zijazo na mambo yakiwa mazuri kila mtu atamfahamu waziwazi.”
TIBA YA TUMBO ILIANZIA INDIA
Mwaka jana Wema alisafiri kwenda nchini India, ambapo Mei 29, mama yake mzazi aitwaye Miriam Sepetu aliiambia Mahakama ya Kisutu jijini Dar iliyokuwa ikisikiliza kesi ya Wema ya matumizi ya dawa ya kulevya kuwa mwanaye hataweza kufika siku hiyo shaurini kwa sababu amekwenda nchini India kwa matibabu.
Kauli hiyo ilizidisha minong’ono ya kwamba Wema alikwenda huko kutibu matatizo yake ya tumbo la uzazi na kwamba msanii huyo aliporejea na kuulizwa na vyombo vya habari vya Global Publishers alikiri kwenda huko kwa matibabu.
Aliongeza kuwa, madaktari wa huko waligundua kuwa ana tatizo la tumbo na kumfanyia upasuaji na aliporejea aliwekwa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake nchini ambao ndiyo waliomhakikishia kuwa sasa amepona na anaweza kuzaa.
SAFARI YA WEMA KUSAKA MTOTO
Wengi walimtazamia Wema kuwa safari yake ya uhusiano wa wazi wa kimapenzi kwa baadhi ya wanaume ingemfikisha kwenye hatua ya kupata mtoto kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mastaa wenzake kama Aunt Ezekiel (aliyezaa na Mose Iyobo) au Hamisa Mobeto (aliyezaa na Diamond), lakini haikuwa hivyo.
Ingawa Wema alipokuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba ilivuma tetesi kuwa alinasa ujauzito, lakini ulichoropoka.
Baada ya hapo Wema alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa wazi na Jumbe Yusuf, Charles Gabriel ‘Chaz Baba’, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Nagari Kombo na Idris Sultan ambao hakuweza kupata nao mtoto.
AOMBEWA HERI
Baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiguswa na kauli za Wema kutamani mtoto, wamekuwa wakimwambia atulie na kusubiri siku ambayo Mungu amempangia kupata uzao.
Siku za hivi karibuni mashabiki wake wengi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii wamekuwa wakimuombea heri Wema ili naye apate furaha ya kuitwa mama.
GPL
No comments:
Post a Comment