Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Mfaume Kizigo akizungumza na wananchi wa wakati wa ufunguzi wa chanjo katika kijiji cha Minazini.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Mfaume Kizigo akiwa na mtoto aliyepata chanjo wakati wa ufunguzi wa chanjo katika kijiji cha Minazini.
NA YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Mfaume Kizigo amewataka wananchi Wilayani Namtumbo kuhakikisha wanawapeleka watoto wao waliochini ya miaka mitano kupata chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya Wilayani humo.
Akiongea na wananchi wa kata ya minazini katika ofisi ya serikali ya kijiji cha Minazini Mkuu wa wilaya huyo aliwataka wananchi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ya ugonjwa wa Surua,Polio na Rubella ili kuwakinga na kuambukizwa na magonjwa hayo.
Aidha Mkuu wa wilaya huyo aliwathibitishia wananchi na kuwatoa hofu kuwa wasiwe na hofu yoyote kwani chanjo hizo zimethibitishwa na shirika la afya ulimwenguni , wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto kuwa ni salama .
Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Namtumbo Godwin Luta alimthibitishia mkuu wa wilaya huyo kuwa wataalamu wa afya wilayani humo wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwapatia watoto chanjo katika vituo vya kutolea huduma ili kuwakinga na magonjwa ya surua Rubella na Polio.
Luta alidai mwitiko wa wananchi kuwapatia chanjo watoto waliochini ya miaka mitano Wilayani humo umekuwa mkubwa kutokana na wananchi hao kuelewa umuhimu wa chanjo hizo na kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za afya .
Adinani Nyoni mkazi wa minazini alisema elimu iliyotolewa na wataalamu wa afya na wataalamu wenyewe kuonesha mfano kwa kuwapatia chanjo watoto wao iliondoa woga kwa wananchi na kusababisha wananchi hao waondoe hofu na kujitokeza kuwapeleka watoto wao kuwapatia chanjo hizo.
Watoto 637 walipatiwa chanjo ya Surua ikiwa wanaume 227 na wanawake 410 na waliopatiwa chanjo ya polio ni 692 ikiwa wanawake 330 na wanaume 362 katika uzinduzi wa chanjo hiyo katika viwanja vya ofisi ya kijiji cha Minazini .
No comments:
Post a Comment