ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 24, 2019

Muasisi wa CUF (Mzee Mapalala) Afariki Dunia

MWANASIASA mkongwe nchini Tanzania na mwanzilishi wa Chama cha Wananchi, Mzee James Mapalala amefariki dunia jana Jumatano Oktoba 23, 2019, saa 4:30 asubuhi katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mtoto wa Mzee Mapalala, Bernard James amethibitisha kutokea kwa kifo cha baba yake na kusema alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Kairuki tangu wiki mbili zilizopita baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kupumua.

“Alikuwa hospitali tangu wiki mbili zilizopita baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kupumua. Familia imekusanyika nyumbani Kinondoni kupanga ratiba ya mazishi,” amesema James.

Mapalala aliyezaliwa Februari Mosi, 1936 ameacha mke na watoto kadhaa. Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza waliojitosa kudai mfumo wa vyama vingi urejeshwe nchini Tanzania.

Kufuatia madai hayo, Mapalala alifungwa miaka miwili mkoani Lindi kuanzia mwaka 1986 hadi 1989 na baada ya kutoka aliwekwa kizuizini kwa kipindi cha mwaka mmoja katika kisiwa cha Mafia baada ya kuanzishwa chama cha siasa wakati sheria ilikuwa hairuhusu.

Alianzisha Chama cha Wananchi (CCW) mwaka 1991 na baadaye kiliungana na chama cha Zanzibar – Kamahuru na mwaka 1993 kuzaliwa Chama cha Wananchi (CUF). GPL

No comments: