ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 15, 2019

Tekinolojia Kuleta Ufanisi Mkubwa Katika Sensa ya Mwaka 2022, Mtakwimu Mkuu wa Serikali.

 Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akizungumza na Afisa Mtendaji, Kata ya Kondoa Mjini Samson Mtui alipofika Ofisini kwake kujitambulisha kabla ya kuanza ziara ya kukagua maendeleo na ubora wa kazi ya kutenga maeneo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022
 Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akisikiliza maelezo kutoka kwa Mrasimu ramani Emmanuel Mahemba wakati wa ziara ya kukagua kazi ya utengaji maeneo katika Mtaa wa Mnarani, Kata ya Kondoa Mjini mkoani Dodoma.  Kulia ni Mrasimu Ramani Galos Mbedule.
 Mkuu wa Kitengo cha Mfumo wa Taarifa za Kijiografia Ofisi ya Taifa ya Takwimu Benedict Mugambi akitoa maelezo namna maeneo ya kuhesabia watu yanavyotengwa na taarifa za taarifa za kijiografia zinavyokusanywa. Wengine ni warasimu ramani na kwa nyuma ni Meneja wa Takwimu Mkoa wa Dodoama Iddi Mruke.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akitoa maelekezo kwa timu ya warasimu ramani wanafanya kazi ya kutenga maeneo huko wilayani Kondoa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema matumizi ya tekinolojia za kisasa zitaleta ufanisi mkubwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 hivyo kuipatia nchi Takwimu za uhakika zaidi na kwa wakati kuliko Sensa zilizopita.

Dk. Chuwa alieleza hayo jana wakati alipotembelea wilaya ya Kondoa kukagua maendeleo na ubora wa kazi katika zoezi ya kutenga maeneo katika mtaa wa Mnarani wilayani Kondoa ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

“Lengo letu ni kufanya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa Ufanisi mkubwa na nimekuja hapa kukagua na kutathmini ubora wa kazi ya kutenga maeneo katika wilaya yenu” Dk. Chuwa alimueleza Afisa Mtendaji, Kata ya Kondoa Mjini Samson Mtui alipofika Ofisini kwake kujitambulisha.
Wakati wa ukaguzi huo Dk. Chuwa alioneshwa namna maeneo hayo yanavyopimwa na kuwekewa mipaka pamoja na namna taarifa zinavyohifadhiwa katika Kishikwabi (tablet) ambazo zitatumika wakati wa kuhesabu watu tofauti na Sensa zilizopita ambapo Wadadisi walikuwa wakitumia ramani zilizochorwa katika karatasi. 

Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Taarifa za Kijiografia katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Benedict Mugambi alimueleza Mtakwimu Mkuu kuwa kwa kutumia Kishikwambi Mdadisi atafanya kazi yake ya kuhesabu watu katika eneo lake tu na hataweza kuingia eneo la mwenzake.
“Mdadisi akitoka nje ya eneo lake Kishikwambwi kitamuonesha alama kuwa anaingia eneo silo lakini zaidi Dodoso halitaweza kufunguka hivyo hataweza kufanya kazi” alieleza Mugambi. 

Dk. Chuwa alibainisha kuwa matumizi hayo ya tekinolojia yatapunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha watu wanaosahaulika kuhesabiwa wakati wa zoezi la kuhesabu watu.
Katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 kiwango cha watu waliosahaulika kuhesabiwa kilikuwa asilimia 5 ambacho hata hivyo ni cha chini ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

Kwa mfano, katika Sensa iliyopita nchini Afrika Kusini kiwango cha watu waliosahaulika kuhesabuwa kiliwa zaidi ya asilimia kumi. 
 “Tunataka kile kiwango cha asilimia 5 cha waliosahauliwa kuhesabiwa mwaka 2012 kiondoke katika Sensa ijayo ili tupate takwimu halisi na kuongeza ufanisi katika upangaji wa mipango yetu ya maendeleo” Dk. Chuwa alisisitiza.

Awali, akitoa taarifa ya kazi, kiongozi wa timu hiyo Mrasimu Ramani Jerve Gasto wa NBS alieleza kuwa hadi sasa vijiji vyote 84 katika Halmashauri ya Kondoa Vijijni tayari vimetengewa maeneo ya kuhesabia watu na taarifa zote muhimu zimeshachukuliwa na kuweka katika ramani.
Kwa upande wa Halmashauri ya Kondoa Mjini, Gasto alieleza kuwa kazi imeanza na wamekamilisha mtaa mmoja wa Mnarani kati ya mitaa 36 na kuongeza kuwa kazi hiyo inatarajiwa kumalizika baada ya siku kumi.
Kuhusu taarifa zilizokusanywa alieleza kuwa ni za huduma za jamii kama elimu, maji na afya, shughuli za uzalishaji kama viwanda na ofisi za serikali na huduma za kiroho. 

Gasto alieleza kuwa mwitikio wa wananchi ni mzuri na wamekuwa wakiwapa ushirikiano wakati wote wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao na kuwashukuru viongozi wa wilaya kwa kuwa nao bega kwa bega tangu walipoanza kazi hiyo wilayani humo.  
Hata hiyo alieleza kuna changamoto kadhaa wanazopambana nazo wakiwa kazini ikiwemo baadhi ya wananchi kuingia katika mapori ya hifadhi na utata wa mipaka katika baadhi ya vijiji. 

Kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu wilayani Kondoa ilianza tarehe 16 Septemba, 2019 na kushirikisha warasimu ramani kutoka NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) na wataalamu wa mipango miji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Watalamu hao wamegawanyika katika timu tano zenye watu watatu kila moja na kwa mujibu wa Gasto timu ya sita inatarajiwa kujiunga nao sasa kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa.

No comments: