Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akizungumza na Balozi wa Norway nchini Bi Elisabeth Jacobsen alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
Mshauri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa Norway Bi Ingvild Langhus (kulia) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo ya Balozi wa nchi hiyo Bi Elisabeth Jacobsen na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akiagana na Balozi wa Norway nchini Bi Elisabeth Jacobsen mara baada ya kufanya nae mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Bi Elisabeth Jacobsen.
Pamoja na masuala mbalimbali wamezungumza namna ya kuendeleza ushirikiano katika miradi ya hifadhi na usimamzi wa mazingira nchini ukiwemo wa Kupunguza Hewa ya Ukaa na Kupunguza Ukataji Miti (REDD+) wenye thamani ya Dola za Marekani 1,096,830 ambapo Serikali ya Tanzania na Norway zipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kuingia makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wake.
Akizungumza na Balozi huyo, Waziri Simbachawe alisema kutokana na umuhimu wa mazingira ipo haja ya shule zote kufundisha somo la mazingira kuanzia elimu ya msingi ili wanafunzi wawe na uelewa mkubwa wa sekta hiyo.
Alifafanua kuwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 inasema kila taasisi inahusika katika shughuli zote za utunzaji na uhifadhi wa mazingira hivyo shule zinapaswa kufundisha wanafunzi ili wawe na uelewa juu ya dhana hiyo.
"Ipo haja ya kuwekeza kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi kwa kuwapa elimu kuhusu mazingira na kwa kufanya hivi tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutunza mazingira kwani wanahitaji kuwa na uelewa wa mambo yanayohusiana na mazingira kwa ujumla," alisema Simbachawene.
Aidha Waziri Simbachawene amezungumzia hatua mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika utunzaji wa mazingira kupitia Ofisi yake ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.
Alisema kuwa Ofisi yake imewahi kuwashindanisha wadau kutengeneza majiko mbadala ambayo hayatumii kuni na mkaa hivyo kusaidia kuepusha vitendo ya ukataji miti.
Katika hatua nyingine Balozi Jacobsen alipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki na kusema hatua hiyo ni ya kuigwa na mataifa mengine ili kusaidia kuondosha madhara yanayotokana na matumizi ya mifuko hiyo.
Alishauri katazo hilo liendelee kuibua fursa za ajira kwa wananchi zikiwemo za kutengeneza mifuko mbadala na kusema kuwa ipo haja ya kufanya kazi kwa pamoja katika kuzuia uchafuzi wa mazingira katika bahari.
No comments:
Post a Comment