Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi (AG) akimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Methew Mwaimu wakati yeye na Makamisha wanaounda Tume hiyo walipomtembelea Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kufanya naye mazungumzo.
Sehemu ya Ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakiwamo Makamisha wakati walipomtembelea ( Courtesy Call) Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi akiwa katika picha ya pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakati Ujumbe wa Tume hiyo walipomtembelea Ofisini kwako leo,Jijini Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi ( AG)leo ( jumatano) amekutana na kisha kuwa na mazungumzo na Ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Mazungumzo baina ya AG na Tume hiyo ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Mhe. Methew Mwaimu yamefanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyopo katika Mji wa Kiserikali Mtumba Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji Mstaafu Methew Mwaimu alimueleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwamba, Madhumuni ya ziara hiyo pamoja na masuala mengine, yalikuwa ni kujitambulisha kwake lakini pia kujadiliana na kubadilishana mawazo ya namna Ofisi hizo mbili zinaweza kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Profesa Kilangi, aliishukuru Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora wa kuona umuhimu wa kumtembelea na kubadilishana naye mawazo ikiwa ni muda mfupi tangu kuteuliwa kwao na kuapishwa kwao.
AG ameihahidi tume hiyo ushirikiano madhubuti kutoka katika Ofisi yake.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu na Huduma za Kisheria, Dkt. Gift Kweka.
Itakumbukwa kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mstaafu Methew Mwaimu na Makamisha wake waliteuliwa Mwezi Septemba mwaka huu na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli.
No comments:
Post a Comment