ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, November 12, 2019
JKCI WAFANYA UPASUAJI WA KUTENGANISHA MSHIPA WA DAMU WA KUSAMBAZA DAMU KWENYE MWILI NA KUWEKA MSHIPA BANDIA WA KUSAMBAZA DAMU KWENYE MAPAFU (TRUNCUS ARTERIOSUS)
NA MWANDISHI MAALUM
KWA mara ya kwanza madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kutenganisha mshipa wa damu wa kusambaza damu kwenye mwili na kuweka mshipa bandia wa kusambaza damu kwenye mapafu (Truncus Arteriosus).
Upasuaji huo uliochukuwa muda wa masaa manne na nusu ulifanyika kwa mtoto mwenye umri wa miezi mitano ambaye alikuwa na tatizo la damu safi na chafu kutokea kwenye mshipa wa damu mmoja badala ya mishipa miwili tofauti.
Mtoto huyo alizaliwa na tatizo la kuwa na mshipa mmoja wa damu ambao ulikuwa unapeleka damu kwenye mwili na mapafu kutoka kwenye moyo badala ya mishipa miwili ya “Aorta” ambao unapeleka damu kwenye mwili na “Pulmonary Artery” ambao unapeleka damu kwenye mapafu.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Godwin Sharau alisema wameweza kutengeneza mshipa wa damu bandia ambao unabeba damu chafu kutoka kwenye chumba cha chini cha kulia cha moyo na kupeleka kwenye mapafu ili kutenganisha damu chafu na safi.
Dkt. Sharau alisema, “Katika upasuaji huo tumeweza pia kuziba tundu la moyo na kulitenganisha kutoka kulia na kushoto ili kuweza kusaidia mzunguko wa damu kuwa katika hali ya kawaida. Mshipa huu bandia utadumu kwa muda wa miaka 10 hadi 15 baada ya hapo utabadilishwa na kuwekwa mkubwa zaidi tofauti na wa sasa ambao ni mdogo”,.
“Aina hii ya magonjwa ya moyo ni nadra sana kutokea lakini katika mazingira yetu tumekuwa tukiwaona watoto wenye matatizo kama haya na watoto kama hawa wasipopata matibabu ndani ya miezi sita tangu kuzaliwa kwao wanaweza kupoteza maisha”,.
Dkt. Sharau alisema kwa mwaka huu wamefanya upasuaji wa aina hiyo kwa wagonjwa watatu ambapo wawili walifanyiwa upasuaji katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya wataalamu kutoka nchini Italia na Ujerumani ambapo huyu wa sasa amefanyiwa na madaktari wazawa wa Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Neema Amani ambaye ni mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji huo alishukuru kwa huduma ambayo mtoto wake alipatiwa na kuwaomba wamama wengine ambao wataona watoto wao wanamatatizo ya afya wasikae nao nyumbani wawapeleke Hospitali kwa ajili ya matibabu.
Anasema mwezi wa tisa mwaka huu alipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kutoka Hospitali ya Mwananyamala baada ya kugundulika kuwa na tatizo la moyo kwani mtoto alikuwa na shida ya kubanwa na kifua, kukohoa na kutokwa na jasho jingi hasa wakati wa kunyonya.
“Naishukuru sana Taasisi hii kwani mwanangu hana bima ya afya na sikuwa na hela ya kulipia matibabu ya moyo. Lakini mwanangu ameweza kupatiwa matibabu na sasa anaendelea vizuri na ameruhusiwa kutoka katika chumba cha Uangalizi Maalum”, alisema Neema.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikifanya kambi maalum za matibabu ya moyo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi. Moja ya faida zinazopatikana katika kambi hizo ni kubadilishana ujuzi wa kazi na mafunzo ambayo yamewasadia wataalamu wa Taasisi hiyo kupata elimu na utaalamu wa kisasa wa hali ya juu na hivyo kutoa huduma nyingi za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment