ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 4, 2019

NACTE Yatangaza Awamu Ya Nne Ya Udahili Katika Ngazi Ya Astashahada Na Stashahada Kwenye Vyuo Na Taasisi Mbali Mbali Kwa Mwaka Wa Masomo 2019/2020

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linautangazia umma kwamba limefungua dirisha la udahili kwa AWAMU YA NNE na ya mwisho, kwenye Vyuo na Taasisi zinazotoa programu za Astashahada na Stashahada hapa nchini, zinazotambuliwa na Baraza kuanzia tarehe  1 Novemba, 2019  hadi tarehe 10 Novemba, 2019 ambapo dirisha hilo litafungwa.

Hatua hiyo imekuja kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Vyuo na Taasisi mbalimbali kutaka nafasi zilizo wazi ziweze kujazwa. Kwa kuzingatia hilo, Baraza linatoa wito kwa wahitimu wa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita na wale wote walio na nia na sifa za kujiunga na programu mbalimbali kutumia fursa hii kutuma maombi ya udahili kwenye Taasisi na Vyuo ambavyo bado vinapokea maombi ya udahili katika ngazi ya Astashahada na Stashahada.

Aidha, Vyuo na Tasisisi zitakazohusika kwenye awamu hii, zinaarifiwa kwamba mfumo utakuwa wazi kupokea majina ya wanaodahiliwa ili kufanyiwa uhakiki hadi hiyo tarehe 10 Novemba, 2019. 

Vyuo na Taasisi zinazotaka kubadilisha taarifa za wanafunzi waliowasilishwa na kuonekana kuwa na mapungufu yaliyopelekea kukosa sifa, nazo zinashauriwa kufanya hivyo ndani ya kipindi hicho kuanzia leo tarehe 01 hadi 10 Novemba, 2019.

Ikumbukwe, kwamba uhakiki wa majina yote yatakayowasilishwa utafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 Novemba, 2019, na  matokeo ya uhakiki yatatolewa tarehe 17 Novemba, 2019.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)

No comments: