Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike(kushoto) akiwasili katika Ofisi za Magereza Mkoa wa Dodoma kabla ya kuhutubia Baraza Maalum la Maafisa na Askari kutoka Makao Makuu ya Magereza Dodoma na vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani humo, kulia ni Kamishna wa Magereza anayeshughulika na Huduma za Urekebu, Mhandisi Tusekile Mwaisabila. Baraza hilo limefanyika leo Desemba 31, 2019.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akiongoza Baraza Maalum la kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020. Baraza hilo limehudhuriwa na Maafisa na Askari kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza Dodoma pamoja na vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani humo. Baraza hilo limefanyika leo Desemba 31, 2019 katika Ukumbi wa Gereza Kuu Isanga, Dodoma.
Baadhi ya Askari wa kike wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali vya Magereza ya Mkoa wa Dodoma wakisikiliza hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike (hayupo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu katika Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Benezeth Bisibe akitolea ufafanuzi masuala mbalimbali ya madeni ya watumishi wa Jeshi hilo yaliyoulizwa na Maafisa na Askari kutoka vituo vya magereza Mkoani Dodoma(hawapo pichani) katika Baraza hilo.
Kamishna wa Magereza anayeshughulika na Huduma za Urekebu, Mhandisi Tusekile Mwaisabila akitoa neno fupi mbele ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike(katikati meza kuu) katika Baraza la kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020(kushoto) ni Naibu Kamishna wa Magereza, John Masunga. Baraza hilo limefanyika leo katika Ukumbi wa Gereza Kuu Isanga Mkoani Dodoma(Picha zote na Jeshi la Magereza).
Na ASP Lucas Mboje, Dodoma;
JESHI la Magereza limejipanga kwa mwaka 2020 kuendelea na utekelezaji wa jukumu la uzalishaji wa chakula cha kutosha cha wafungwa kwa kutumia rasilimali zilizopo katika Jeshi hilo ili kufikia adhma ya Serikali ya awamu ya tano kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.
Akizungumza na Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020 leo jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa Jeshi hilo tayari limejiwekea mkakati maalum wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.
Katika kulifanyia kazi suala hilo, Kamishna Jenereali Kasike amesema kuwa mavuno yameongezeka katika msimu wa kilimo 2018/2019 ambapo Jeshi hilo limeweza kuzalisha chakula cha wafungwa katika magereza kumi(10) ya kimkakati(Songwe, Mollo, Ludewa, Arusha, Pawaga, Idete, Kitete, Isupilo, Kitai na Kitengule).
“Kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza(SHIMA), Jeshi limeweza kulisha unga wa mahindi kwa wahalifu magerezani kwa kipindi cha mwaka mzima katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara, Rukwa, Njombe na Katavi. Aidha, katika mikoa mingine Shirika limeweza kulisha unga kwa miezi mitatu hadi sita”, amesema Kamishna Jenerali Kasike.
Ameongeza kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya magereza ambapo Jeshi hilo tayari limekamilisha andiko linalohusu mapindizi ya kilimo na tayari limewasilishwa serikalini katika hatua mbalimbali za ngazi ya maamuzi.
Akizungumzia mafanikio mengi ya kujivunia kwa mwaka 2019 Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa miongoni mwa maafisa na askari katika kuishi na ajenda mahususi ya Jeshi hilo kuhusu umuhimu wa kubadilika kimtizamo, kifikra na utendaji kama nguzo ya mabadiliko katika Jeshi hilo.
“Naomba nisistize kuwa bado tuendelee kuishi na ajenda hii ya mabadiliko ya kimtizamo na kifikra katika mwaka mpya 2020 tunaoutarajia kuuanza muda mfupi ujao kwa kufanya kazi kwa weledi, ubunifu katika maeneo yetu ya kazi. Tradition die hard”, amesisitiza Kamishna Jenerali Kasike.
Mafanikio mengine aliyoyaainisha ni pamoja na utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa, ujenzi wa nyumba za watumishi wa Jeshi hilo katika maeneo mbalimbali nchini kwa njia ya ubunifu, udhibiti wa uingizaji wa vitu visivyoruhusiwa magerezani kwa kufunga CCTV camera katika baadhi ya magereza pamoja na kuhakikisha kuwa wafungwa waliopo magerezani wanafanya kazi.
“Shirika la Magereza limefanikisha utaratibu wa kuingiza miradi yake yote katika mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali(GePG) na hivyo kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali. Pia, Shirika hilo limeweza kutoa mchango wake Serikalini kiasi cha Tsh. Milioni mia moja na therasini kwa mwaka 2019”, ameainisha Kamishna Jenerali Kasike.
Aidha, pamoja na mafanikio hayo Kamishna Jenerali Kasike amebainisha changamoto zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti, uhaba wa vitendea kazi mbalimbali kama vile magari, vyombo vya mawasiliano, pia changamoto za makazi na uchache wa nguvu kazi ya maafisa na askari katika Jeshi hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amehitimisha hotuba yake leo jijini Dodoma kwa kuwatakia heri ya mwaka mpya 2020 maafisa, askari pamoja na watumishi wote wa Jeshi hilo na amewataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya kazi, Dira na Dhima ya Jeshi hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment