ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 23, 2019

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI, PHAUSTINE KASIKE AHIMIZA WAFUASI WAKE KUZINGATIA NIDHAMU JESHINI

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Phaustine Kasike akizungumza katika kikao na Maafisa na askari wa vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya utendaji kazi, maadili ya kazi, nidhamu na mikakati mbalimbali ya Jeshi ikiwemo ya Kilimo, viwanda na ufugaji. Kikao kazi hicho kimefanyika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(hayupo pichani) kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya utendaji kazi, maadili ya kazi, nidhamu na mikakati mbalimbali ya Jeshi ikiwemo ya Kilimo, viwanda na ufugaji.
Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Magereza kutoka katika vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mazungumzo ya kikao kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Phaustine Kasike jana Desemba 20, 2019(Picha zote na Jeshi la Magereza).

Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amewaasa Maafisa na askari wote wa Jeshi hilo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia nidhamu ya kazi na kufuata taratibu zilizopo ndani ya Jeshi.

Amesema hayo jana katika kikao kazi na Maafisa na askari wa vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya utendaji kazi, maadili ya kazi, nidhamu na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Jeshi hilo ikiwemo mpango mkakakti wa kilimo, uwekezaji katika viwanda na ufugaji.

Kamishna Jenerali Kasike amesisitiza kuwa nidhamu ni muhimu Jeshini na amesema hakuna mtu aliye juu ya nidhamu kwani msingi wa Jeshi lolote lile ni nidhamu.

"Taswira ya Jeshi la Magereza inategemea zaidi utekelezaji mzuri wa majukumu yenu kwa kuzingatia nidhamu na maadili ya kazi. “Kila mmoja lazima atimize wajibu wake kikamilifu kwa kutumia uweledi, ubunifu na kuzingatia nidhamu ya kazi”, alisisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa wapo baadhi ya maafisa na askari ambao wanamatatizo ya kinidhamu na hawataki kubadilika hali ambayo inaharibu taswira ya Jeshi hilo katika jamii.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike amekemea tabia ya kutokufuata taratibu za uwasilishaji wa malalamiko kupitia utaratibu uliopo ndani ya Jeshi hilo kwa baadhi ya maafisa na askari kwani tabia hiyo inachangia sana katika kushuka kwa nidhamu ndani ya Jeshi.

“Jeshi ambalo halina nidhamu ni sawa na genge la wahuni ambao wamevaa sare za Jeshi. Hivyo natoa wito kwa Maafisa na askari wenye matatizo ya kinidhamu wajisahihishe na kujirekebisha ili kuendana na misingi ya Jeshi”, aliongeza Jenerali Kasike.

Pia, amesema kuwa atahakikisha Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza (SHIMA) linajidhatiti zaidi katika miradi yake ili kujiimarisha katika kufanya shughuli za kibiashara hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Julius Ntambala amemhakikishia Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza kuwa atahakikisha kuwa Maafisa na askari katika Mkoa wake wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo katika uendeshaji wa Jeshi hilo.

No comments: