Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (aliyevaa kiraia), akimvisha cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza,Revocatus Kilanga baada ya kuhitimu Mafunzo ya Ngazi ya Juu wakati wa Mahafali yaliyofanyika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni(aliyevaa kiraia),akikagua gwaride lililoandaliwa wakati wa Sherehe ya Kuhitimu Mafunzo ya Ngazi ya Juu iliyofanyika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga jijini Dar es Salaam.(Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
Na Abubakari Akida
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Miradi yote ya Ujenzi itakayokuwa inatekelezwa ndani ya vyombo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi sasa itafanywa na wakandarasi kutoka Jeshi la Magereza na Polisi ili kuweza kutumia vikosi kazi hivyo ambavyo vimesheheni wataalamu wa kada hiyo huku agizo hilo likienda sambamba na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano kubana matumizi na kuokoa fedha nyingi za walipa kodi zilizokuwa zikipotea.
Masauni ameyasema hayo wakati akihutubia katika Sherehe za Kufunga Mafunzo ya Maafisa Ngazi ya Juu yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga jijini Dar es Salaam huku akiwaasa wahitimu hao kwenda kusimamia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika maeneo yao ya kazi.
“Natumia fursa hii kutoa maelekezo kwa taaasisi zote zilizopo ndani ya Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi ni marufuku miradi ya ujenzi wa vyombo vilivyopo chini ya wizara kutafuta mjenzi au mkandarasi kutoka nje ya vyombo vyetu hii,inatakiwa tuanze kuvitumia vikosi hivi ili tuvijengee imani huko nje na imani yangu inaniambia uwezo huo tunao na tunaweza,Shirika la Uzalishaji mali lazima likiboreshe kikosi hicho cha ujenzi cha magereza ili mwakani kiweze kutoa gawio kwa serikali”
Akizungumza katika sherehe hiyo Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP Faustine Kasike alisema jeshi la magereza limeshaingia katika mkakati wa kujitosheleza kwa chakula ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli na tayari magereza kumi ya kimkakati yashaanza kutoa matunda huku akiweka wazi mkakati wa kuongeza vitendea kazi katika magereza hayo kumi ya kimkakati.
“Jeshi la Magereza sasa limejipanga kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji na kiuendesahji ili kuweza kuendana na kasi ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli,moja ya sehemu inayofanyiwa maboresho ni sehemu ya mafunzo ili tuweze kuwa na ufanisi na kasi,kwahiyo kozi unayoifunga leo imeandaliwa kwa mtazamo huo na tuna hakika wahitimu hawa watakua chachu ya mabadiliko hayo” alisema Kamishna Kasike
Akisoma Risala kwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Wahitimu,mmoja wa wahitimu amesema mafunzo hayo yamewapa uweledi hasa katika kipindi hiki chakuchangia uchumi wa nchi ikiwemo kujitosheleza kwa chakula kwa Jeshi la Magereza ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali ya Awamu ya Tano huku wakiahidi kutumia elimu waliyoipata kulibadilisha jeshi katika maeneo ya kazi watakayopangiwa.
Jumla ya wahitimu 115 wamehitimu mafunzo hayo ya Maafisa Ngazi ya Juu ambapo watapangiwa sehemu mbalimbali za kazi ili kwenda kuboresha utendaji katika maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment