ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 18, 2019

MCHAKATO MABADILIKO YA SERA YA JINSIA NCHINI WAENDELEA JIJINI DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya Bi. Grace Mwangwa wa kwanza kulia Afisa Tawala Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam B. Yokobeti Malisa pamoja na Profesa Linda Mhando wakifuatilia jambo wakati kikao kazi cha wadau wa sera ya jinsia hiyo kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro.
Baadhi ya Wadau walioshiriki kikao kazi cha wadau wa sera ya jinsia hiyo kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro jana Jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakifuatilia jambo wakati kikao kazi cha wadau wa sera ya jinsia hiyo kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro jana Jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi wetu Dar.

Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii inakutana pamoja na wadau Jijijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya mapitio ya Sera ya Jinsia ya Mwaka 2000 pamoja na mkakati wa utekelezaji wake wa mwaka 2005 na kuifanyia tathimini ili iweze kuendana na mabadiliko yaliyopo kwa sasa.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa sera ya jinsia hiyo kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya Bi. Grace Mwangwa amesema mapitio ya Sera hiyo ni shikirikishi kutoka katika makundi yote ili sera hiyo iweze kugusa kila mmoja katika jamii.

Aidha Bi Mwangwa ameongeza kuwa Sera hiyo imekuwepo kwa kipindi cha takribani miaka 19 hivyo kwa sasa ni wakati sahihi kwa Serikali kufanya mapitio ya Sera hiyo na kuifanyia maboresho ili iweze pia kuendana na mabadiliko yaliyopo ya sayansi na teknolojia pamoja na mabadiliko ya sheria zilizopo kuhusu maendeleo ya jinsia Nchini.

Bi. Mwangwa amewataja wadau muhimu katika kuhakikisha Sera hiyo inafanyiwa marekebisho kuwa ni wawakilishi wa wanawake, maafisa ustawi wa jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wadau kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na wawakilishi wa watu wenye mahitaji maalum katika jamii kwa lengo la kuhakikisha hakuna kundi hata moja katika jamii litakalo achwa nyuma katika mababoresho ya sera hiyo.

Naye Afisa Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dar es Salaam Bi,Yokobet Malisa amewataka wadau wa kikao kazi hicho kuangalia namna bora ya kuhakikisha makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu masuala yao yanazingatiwa katika mabadiliko ya Sera hiyo kwa kuzingatia kwamba nia gizo la serikali kuhakikisha makundi haya yanawezeshwa kiuchumi.

‘’Mnafahamu kwa sasa kuwa serikali imetoa agizo la kuzitaka Halmashauri zote Nchini kutenga asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya kusaidia wanawake, vijana, na walemavu na nina uhakika makundi yote haya yapo hapa hivyo hakikisha kwamba Sera hii inazingatia pia matakwa ya mahitaji ya makundi maalum katika jamii.

Mshauri Mwelekezi wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Jinsia Profesa Linda Mhando amesema Tanzania kwasasa imesaini makubaliano mbalimbali ya kimataifa ambayo hayakuwepo wa katika sera ya awali hivyo ni wakati muhafaka wa kufanya mabadiliko katika sera hiyo ambayo amedai imepitwa na wakati hivyo kuifanyia mabadiliko ili iweze kuendana na makubaliano ya kimataifa yaliyoko.

Profesa Mhando ameongeza kuwa maoni ya Sera hiyo mpaka sasa yanaendelea mpaka hatua ya vijiji na kata kwa lengo la kuahakikisha wanapata maoni mengi zaidi yatakayoweza kusaidia kupata maoni ya kila mtu ikiwemo marekebisho ya mkakati wa utekelezaji wa Sera hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Jinsia.

Mapatio ya Sera ya Jinsia na mchakato wa ukusanyaji maoni yanaendelea Jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha Wadau wa Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro na pia mchakato huo utaendelea kwa Kanda ya Kaskazini kwa lengo la kupata maoni zaidi yatakayotumika kuboresha Sera hiyo muhimu kwa maendeleo ya Jinsia Nchini.    

No comments: