ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 21, 2019

Mikusanyiko misibani hadi kibali cha DC

Wakazi wa Mtumba wakimzika marehemu Edward Mabumba ambaye msiba wake umekuwa watu 55 walilazwa hospitali baada ya kudaiwa kula chakula chenye sumu. Picha na Habel Chidawali

By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imetoa amri ya muda kuzuia mikusanyiko kwenye misiba mtaa wa Mtumba jijini hapa. Amri hiyo inawataka wakazi hao kupata kibali cha mkuu wa wilaya kukusanyika kwenye msiba wowote mtaani hapo.

Hatua hiyo inatokana na watu 55 kulazwa hospitali kwa kuugua ugonjwa wa tumbo ghafla baada ya kula chakula kwenye msiba.

Pia, amri hiyo ilitolewa kutokana na kujirudia kwa matukio ya aina hiyo kwenye mtaa huo, kwani hilo ni tukio la pili baada ya mwaka 2017 watu wawili kufariki kwa madai ya kula chakula kilichohisiwa kuwa na sumu msibani huku wengine wakilazwa hospitali.

Akizungumza na Mwananchi jana, ofisa afya wa Jiji la Dodoma, Abdallah Mahinya alisema kibali hicho hakiombwi Polisi bali kinatoka kwa mkuu wa wilaya.

Mahinya alisema timu ya afya ya jiji ndiyo walitoa pendekezo la kuwapo utaratibu huo eneo hilo, huku wakisubiri majibu ya sampuli za vipimo vilivyochukuliwa kwa watu hao. “Watu wa afya tulimshauri mkuu wa wilaya bahati akawa msikivu na ametoa amri hiyo hadi hapo tutakapomshauri vinginevyo,” alisema Mahinya.

Naye mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi alipoulizwa suala hilo alituma ujumbe mfupi kwenye simu akikiri kuwapo kwa agizo hilo na imechukuliwa kwa ajili ya usalama wa watu.

Awali, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mtumba, Robert Chigugude aliliambia gazeti hili kuwa kwa sasa hakuna ruhusa ya kukusanyika misibani au wakati wa mazishi mtaani hapo.

Diwani wa Mtumba, Edward Maboje alisema gharama za kuwahudumia watu 55 walioathirika ni Sh5.2 milioni.

No comments: