Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kukutana na serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kusikiliza malalamiko yao na kuyapatia ufumbuzi.
Agizo hilo la limetolewa leo Jumatatu Desemba 16, 2019 na Naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia hiyo, Willium Ole Nasha alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni saa chache kupita tangu Daruso kutoa saa 72 kwa HESLB kutoa mikopo kwa wanafunzi waliokosa, vinginevyo watakutana nje ya ofisi za bodi hiyo zilizopo Mwenge Dar es Salaam Alhamisi ya Desemba 19, 2019.
Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Daruso, Judith Mariki alisema wamefikia uamuzi huo baada ya changamoto ya kukosekana kwa mikopo kwa wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza tangu chuo kifunguliwe huku baadhi ya wanafunzi wanaoendelea wakikatwa fedha zao.
“Tumesikia malalamiko yao na tayari tumeagiza uongozi wa bodi ya mikopo kwenda kuwaeleza kipi kilichosababisha tatizo hilo na hakika wataeleweshwa na wataelewa,” amesema Ole Nasha
Amesema Serikali imetoa Sh125 bilioni katika awamu ya kwanza kwa wanufaika wote lakini katika suala hilo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna wanafunzi wamebadili kozi na wengine kukataa rufaa, kurudia mitihani ndilo limechelewesha fedha hizo kuwafikia.
“Imani yangu hilo suala litamalizika na hizo saa 72 walizozitoa hazitafika huko. Mchana huu wanakutana na baada ya hapo tutawajulisha,” amesema
Mwananchi limezungumza na Makamu wa Rais wa Daruso, Jackile Ndombele ambaye amesema wamefikia uamuzi wa kutoa saa 72 baada ya kufanya vikao na HESLB mara kadhaa lakini suala hilo halipati ufumbuzi.
“Tumefikia kuchukua uamuzi huu mgumu baada ya kufanya vikao zaidi ya vitatu na bodi lakini hakuna hatua inayochukuliwa na wanafunzi wamekuwa wakiona Daruso inawakingia kifua bodi ya mikopo,” amesema Jackline
Mwananchi limezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru ambaye amesema wamepokea maelekezo ya wizara na wanakwenda kukutana na uongozi wa UDSM ikiwamo Daruso ili kulishughulikia suala hilo.
Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema alikuwa kikaoni a anafuatilia suala hilo ikiwamo barua hiyo ya Daruso na baadaye atakuwa na nafasi nzuri ya kulizungumzia.
No comments:
Post a Comment