Viongozi hao ambao kwa muda mrefu walikuwa katika mgogoro walikubaliana Jumanne katika mji mkuu wa Juba, Sudan Kusini.
Akizungumza katika hafla ya makubaliano hayo Rais Kiir alisema yeye na Machar wamefikia makubaliano ya kuunda Serikali hiyo ambayo imecheleweshwa kwa muda mrefu kwa maslahi ya Wasudan wote.
Kiir na Machar ambaye sasa ni kiongozi wa upinzani walikutana siku tatu zilizopita katika mji mkuu wa Juba ili kumaliza tofauti zilizosalia.
Tofuati hizo ndizo zilizozuia kuundwa kwa Serikali ya muungano kufikia tarehe ya mwisho iliyokuwa imewekwa ambayo ni Novemba 12.
Mwezi uliopita viongozi hao wawili walisogeza mbele muda wa kuunda Serikali ya muungano kwa siku nyingine 100.
Katika mvutano huo viongozi hao walishindwa kukubaliana juu ya mipaka ya maeneo.
Jambo lingene ambalo lilichukua muda mrefu kuelewana ni jukumu la kuwaunganisha wapiganaji wake.
Katika harakati za kuwaunganisha, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, alifanya kitendo cha kihistoria ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa kupiga magoti na kuibusu miguu ya viongozi hao wa Sudan Kusini.
Baada ya hatua hiyo ya kuwasihi wasirejee katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, viongozi hao ambao walikuwa mahasimu wa kisiasa wamefikia makubaliano hayo ya juzi.
No comments:
Post a Comment