ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 7, 2020

KAULI YA MEMBE BAADA YA KUHOJIWA , AELEZA FURAHA YAKE


By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

Dodoma. Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Bernard Membe amehojiwa kwa saa tano na kamati ya maadili ya CCM mjini Dodoma, kubainisha kuwa mahojiano hayo yamemuacha na furaha ya ajabu.

Membe aliyefika ofisi za makao makuu ya CCM maarufu ‘white house’ saa 3 asubuhi na kutoka saa 8:43 mchana, amesema baada ya kuhojiwa anakwenda na mkewe katika hoteli moja ambayo haijulikani kula chakula cha mchana, kisha kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam.

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyoketi Desemba 13, 2019 iliagiza makada watatu wa chama hicho waitwe na kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho baada ya kutuhumiwa kwa makosa ya kwenda kinyume na taratibu za chama.

Leo kahojiwa Membe, wengine watakaohojiwa ni makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba.

Akiwa ameketi kwenye gari aina ya Range Rover baada ya kutoka kuhojiwa, Membe aliulizwa mambo kadhaa na waandishi wa habari kuhusu mahojiano hayo, “tulikuwa na mkutano wa saa tano ya mijadala mizuri, mikubwa ya kitaifa inayohusu CCM na nchi yetu. Nimekuwa mtu wa furaha kubwa ajabu kwa sababu nimepata nafasi nzuri ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa.

“Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu kilitaka kuyajua. Nimepata nafasi nzuri ya kutoa mawazo ya yale mambo ambayo niliombwa kutoa mawazo,” amesema Membe.

Ameongeza, “sasa hivi mimi na mke wangu tunakwenda kula chakula kizuri katika hoteli moja ambayo haijulikani na baada ya hapo nitaanza safari kwenda Dar es Salaam.”\

“Ninawaambia tu safari ya kuja Dodoma ilikuwa ya manufaa makubwa sana kwangu, kwa chama na kwa Taifa letu. Mengine yatakuwa yakipatikana kidogokidogo nikishiba.”

Alichokisema Membe jana


Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam jana, Membe amesema ana amini kikao hicho kitakuwa kigumu huku akitumia neno ‘itategemea’, akimaanisha uamuzi utakaotolewa na kamati hiyo baada ya kumhoji.

Juzi, ikiwa ni siku 52 zimepita tangu CCM kutangaza kuwaita wanachama wake watatu kuhojiwa, Membe aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, “hatimaye, nimepokea barua ya kuitwa kwenye kikao cha kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu jijini Dodoma.”

Katika akaunti ya Twitter, ambayo mara kadhaa imekuwa ikitoa taarifa kuhusu mwanadiplomasia huyo, kuliandikwa: “Kikao kitafanyika Februari 6, 2020 saa 3 asubuhi kwenye jengo la White House. Nitahudhuria bila kukosa na bila kuchelewa! Stay tuned!”

Alipoulizwa na mtangazaji aliyekuwa akimhoji kama atakuwa tayari kwa uamuzi wowote, Membe alijibu kwa ufupi, “Itategemea.”

Kuhusu jopo litakalomfanyia mahojiano, amesema kikao hicho kitaongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, akidai mahojiano kuwa mazuri, yenye uwazi huku akitamani ushiriki wa wanahabari katika mahojiano hayo.

“Ninawaambia Watanzania, kesho ni siku muhimu sana, nilikuwa ninaisubiri sana kukutana na hii kamati na ninamuomba Mungu anijaalie niwepo katika kamati kwa sababu nitapata nafasi ya kuzungumza na wanakamati mambo wasiyoyajua na wanayoyajua.”

“Kwa hiyo kesho (leo) saa tatu asubuhi nisikosekane kwenda , niko sasa safarini kwenda Dodoma ili kesho (leo) tukazungumze. Kamati itasikiliza hoja na watatoa mapendekezo kwa halmashauri kuu ya Taifa ambayo itaamua kutoa uamuzi wowote, nadhani uamuzi utatoka mwishoni mwa mwezi huu Februari au Machi,” amesema Membe.

Baada ya mahojiano hayo, Membe amesema atakuwa tayari kuzungumza na wanahabari kwa kuwa suala hilo limekuwa wazi kwa umma tangu mwanzo.

Membe, Kinana na Makamba waliibua mjadala baada ya sauti zao kusikika mitandaoni wakizungumzia mpasuko ndani ya CCM, wameitwa sasa kuhojiwa kujibu tuhuma za kuvunja maadili.

Wakati vigogo hao wakitakiwa kuhojiwa, Halmashauri Kuu ya CCM iliwasamehe na kuwaonya wabunge wake watatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama) ambao kwa nyakati tofauti walimuomba msamaha Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.

Kinana na Makamba walikuwa wamewasilisha malalamiko yao CCM, Julai 14 2019 wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa akiwadhalilisha na ambaye walimuelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Sauti hizo zilizoanza kusambaa mitandaoni baada ya waraka huo wa Makamba na Kinana walioupeleka kwa Katibu wa Baraza la Ushauri wa Viongozi wa CCM, Pius Msekwa kuwa umesambazwa kwenye vyombo vya habari.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, walitumia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalizua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Membe anayedaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na viongozi wa juu wa CCM, ni mara ya pili kufika mbele ya kamati hiyo.

Mara ya kwanza ilikuwa Februari 10, 2014 akiwa na wenzake Ngeleja (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) na Makamba (akiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).

Wengine walioitwa ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliowahi kuwa mawaziri wakuu na Steven Wasira, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais.

Kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la 2017 zimebainisha adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo.

Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.

No comments: