ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 5, 2020

Umeumizwa Moyo wako na Umpendaye


UNAPOZUN-GUMZIA suala la maumivu ya mapenzi, japokuwa huumiza sana hasa kama ulikuwa na mapenzi ya dhati na mwenzi wako na baadaye akaaamua kukugeuka, siyo suala geni hapa duniani. Unapolia leo kwa sababu ya mapenzi, elewa kwamba mamilioni ya watu wanalia kama wewe ingawa tunatofautiana namna ya kukabiliana na maumivu. Lakini cha kujiuliza ni je, mpenzi wako akikuumiza sana, ni sahihi kujiapiza kwamba hutapenda tena?

Ni sahihi kusema kwamba siku hizi hakuna mapenzi ya ukweli kwa sababu tu amekuumiza? Ni sahihi kusema wanaume wote wako hivyohivyo au wanawake wote ndivyo walivyo?

Ukweli ni kwamba, unapovunjika moyo haimaanishi kwamba huo ndiyo mwisho wako wa kupenda. Unapojiapiza kwamba hutapenda tena au hutamwamini mtu tena, ni makosa makubwa kwa sababu kama uliyekuwa naye ameshindwa kuiona thamani ya penzi lako, yupo ambaye atakuthamini na kukuheshimu. Kuna usemi maarufu kwamba mlango mmoja unapojifunga, mwingine huwa unafunguka muda huohuo lakini wengi wetu hupoteza muda mrefu kuutazama ule uliojifunga badala ya kuufuata ule uliofunguka.

Msemo huo una maana kubwa kwenye mapenzi kwamba kama mwenzi wako amekutenda, amekuvunja moyo, amekusononesha na kukufanya ulie, jua kwamba hakuwa ridhiki yako. Huwezi kujua Mungu amekuepusha na nini kwa hiyo badala ya kujiapiza na kukufuru, ni bora ukakubaliana na ukweli, japo huwa inauma sana.

Ukishaukubali ukweli, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupona majeraha ndani ya moyo wako na nakuhakikishia, hata kama ulimpenda vipi huyo uliyekuwa naye, kama amefikia hatua ya kukuumiza na kuuvunja moyo wako, hakuwa riziki yako, endelea kumuomba Mungu kwa sababu yupo ambaye ndiye haswa aliyepangwa kuwa wako.

Upo usemi mwingine kwamba watu wengi huwa hawaoni umuhimu wa kitu mpaka wanapokipoteza, na wakati huohuo huwezi kujua ulichokuwa unakikosa mpaka pale utakapokipata. Yawezekana ulimpenda sana lakini huwezi kujua ulikuwa unakosa nini mpaka utakapokutana na yule mwenye mapenzi ya dhati, ambaye atakuheshimu na kukutunzia penzi lako.

Kinachowaumiza wengi huwa ni matarajio makubwa wanayokuwa nayo kwa wenzi wao. Unapomuonesha mwenzi wako mapenzi ya dhati, haimaanishi kwamba nay eye atakuonesha kama unavyotaka iwe.

Unaweza kupenda sana lakini ukaishia kulipwa mabaya, kitu cha kuzingatia ni kwamba kama umeamua kupenda, penda kwa moyo wako wote na kama unayempenda ni sahihi kwako, utajikuta nafsi yako ikiridhika na utakuwa na furaha.

Unapoweka mategemeo makaubwa kwamba mwenzi wako naye atakupenda katika kiwango sawa na kile unachompenda, ikitokea ameenda tofauti, maumivu yake huwa makubwa sana. Kwa leo ni hayo tu, kwa mada nyingine nzuri za mapenzi, nisikilize katika Kipindi cha The Late Night Show kupitia +255 Global Radio kuanzia saa nne za usiku, kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi. Download App ya 255 Global Radio kupitia simu yako ya mkononi na subiri ikifika saa nne za usiku uungane nami kwenye kipindi kizuri kabisa kinachozungumzia mambo ya kimapenzi na burudani nzuri ya muziki.

GPL

No comments: