ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 1, 2020

MABULA ATAKA MALIPO YA KODI YA PANGO LA ARDHI KWA MITANDAO YA SIMU KUEPUKA CORONA

Na Munir Shemweta, WANMM SIMIYU

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi kufanya hivyo kupitia mitandao ya simu za viganjani ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi ya virusi vya Corona.

Dkt Mabula alitoa tahadhari hiyo juzi wilayani Bariadi mkoani Simiyu alipozungumza na Wakurugenzi na Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu akiwa katika ziara ya kuangalia utendaji kazi wa sekta hiyo sambamba na kufautilia maagizo aliyoyatoa kuhusiaa na sekta ya ardhi.

Alisema, ni vizuri katika kipindi hiki ambacho kuna maambulizi ya virusi vya Corona wamiliki wa ardhi wakachukua tahadhari ya kutokwenda ofisi za ardhi kulipia kodi ya pango la ardhi na badala yake wafanye malipo kwa kutumia mitandao ya simu.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, malipo ya kodi ya pango la ardhi yanaweza kufanyika kwa kutumia mitandao yote ya simu za viganjani pamoja na kutembelea tovuti ya Wizara.

‘’Katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi ya virusi vya Corona wadaiwa pamoja na wale wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi wakafanya hivyo kupitia mitandao ya simu pamoka na kutembelea tovuti ya Wizara ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi’’ alisema Dkt Mabula

Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya Pango la Ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu, Dkt Mabula ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji kodi ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu pamoja na mkoa huo kusifika katika masuala ya uwekezaji.

‘’ Mkoa wa Simiyu mapato yatokanayo na kadi ya pango la ardhi yako chini sana, lengo la makusanyo kwa mkoa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya bilioni 10 lakini kiasi mlichokusanya hadi sasa ni milioni 190 tu sawa na asilimia 9.1, inaonesha hamjawa makini kufuatilia madeni’’ alisema Dkt Mabula

Aidha, Naibu Waziri Mabula alisema hata malengo ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi yaliyowekwa katika baadhi ya halmashauri hayaendani na hali halisi na kutolea mfano wa halmashauri ya Busega kuwa na lengo la kukusanya milioni 30 wakati inadai milioni 343 kutoka kwa wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi.

Kaimu Mkuu wa mkoa wa Simiyu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alimuhakikishia Naibu Waziri wa Ardhi, halmashauri za mkoa huo zitaanza kuwafuatilia wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi sambamba na kuhakikisha viwanja vinaingizwa katika mfumo na kuwahamaisha wananchi kuchukua hati za ardhi ili kuongeza kasi ya makusanyo ya kodi ya ardhi.
Kiswaga alipongeza maboresho mbalimbali yanayofanywa na wizara ya ardhi katika masuala ya utoaji huduma hizo na kutolea mfano uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa kuwa ni moja ya mambo yatakayoleta ufanisi katika sekta ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifuatilia wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi katika mfumo wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za wamiliki wa ardhi katika halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu juzi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Kodi wizara ya Ardhi Denis Masami.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizingumza na Wakurugenzi na Watendaji wa sekta ya rdhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu juzi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga na wa tatu kulia ni Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Simiyu Maganga Simon.
Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu wakiwemo Wakurugenzi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) alipofanya ziara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo juzi.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Festo Kiswaga akizungumza wakati wa kikao baina ya Watendaji wa sekta ya ardhi wa halmashauri za mkoa wa Simiyu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya rdhi katika mkoa huo juzi. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi vifaa kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu Melkizedek Oscar wakati alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo juzi. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Denis Masami (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

No comments: