
MMESIKIA? Ule mchongo wa klabu kuruhusiwa kubadilishwa wachezaji kutoka watatu hadi wanne ndani ya mchezo, sasa ruksa nchini hivyo ni kazi tu kwa klabu kama Simba, Yanga na nyingine kumaliza mambo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubariki.
Mabosi wa TFF na wale wa Kamati ya Waamuzi, wamesema mchongo huo utaanza kutumika ligi itakaporejea baada ya tamko la serikali, kwani kila kitu kipo sawa na timu 20 za Ligi Kuu Bara zijiandae tu kufanya mabadiliko ya wachezaji kwa idadi hiyo kama ilivyopendekezwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na kupitishwa na Bodi Inayopanga Sheria za mchezo huo Duniani (IFAB).
Katika taarifa yake, IFAB imesema wameamua kupitisha sheria hiyo kwa nchi ambazo Ligi zao zimesimama kutokana na ugonjwa wa corona na vile vile kupendekeza ligi ambazo zinatumia teknologia ya mwamuzi msaidizi (VAR) kuacha kutumia kwa kipindi cha kuanza kwa ligi zilizosimamishwa awali.
Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alisema watatekeleza agizo la IFAB, kwani lina lengo lake ni kuziwezesha timu kufanya vizuri katika mechi zake baada ya kukaa muda mrefu bila ya mazoezi kutokana na sababu za ugonjwa wa corona.
“Maamuzi ya IFAB ni maelekezo, hatuna sababu ya kupinga kwani lengo lake ni kujali afya ya wachezaji na hasa kutokana na janga hili la dunia la ugonjwa wa corona. Tumeelekeza kamati yetu ya waamuzi kufanyia kazi,” alisema Kidao.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Israel Nkongo alisema sheria hiyo ya IFAB haina haja ya kuandaa semina kwa vilabu zaidi ya utekelezaji.
Nkongo alisema kilichofanyika ni kwa ajili ya maendeleo ya soka na makocha wanatakiwa kujua idadi ya wachezaji wa kubadilisha (substitutes players) imeongezeka kwa ligi ambazo zipo mbioni kuanza ni watano baadala ya watatu.
“Ni suala la utekelezaji tu na si vinginevyo, sheria inajieleza wazi kuwa ni wachezaji watano, ni maamuzi ya klabu kufanya hivyo au kuacha, Ila Fifa na IFAB wamekwisha pitisha na sisi ni wajibu wetu kutekeleza endapo Ligi itaendelea,” alisema.
No comments:
Post a Comment