ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 21, 2020

KOTEI ATULIZA PRESHA YANGA

By CHARLES ABEL, MWANASPOTI

NI wazi kwamba taarifa za kiungo James Kotei kuvunja mkataba na klabu ya Slavia Mozyr inayoshiriki Ligi Kuu ya Belarus, zimepokelewa kwa shangwe na Yanga inayomuwinda nyota huyo.

Kitendo hicho kinawaweka Yanga kwenye nafasi nzuri kumnyakua Kotei baada ya kufanya naye mazungumzo mara kadhaa ingawa kikwazo kilikuwa mkataba huo ambao sasa umevunjika.

Lakini, pengine taarifa za Kotei kuvunja mkataba zinaweza kuwafanya baadhi kuanza kutilia shaka kiwango chake wakihisi labda uamuzi huo umechukuliwa kutokana na kusugua benchi katika timu hiyo na hata Kaizer Chiefs alikokuwa akiichezea mara alipoachana na Simba.

Hata hivyo, siku moja baada ya kuvunja mkataba huo, Kotei amefichua siri alichukua uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na huduma alizozipata katika timu na sio kwa sababu ya kiwango.

“Unajua nilijiunga na ile timu nikiwa mchezaji huru sasa uongozi haukuwa ukinithamini kama ilivyo kwa wachezaji wengine na baadhi ya huduma nikawa sizipati kama ilivyo kwa wenzangu.

Mfano kuna wakati nilipata majeraha, lakini klabu haikunipatia matibabu sasa kutokana na hilo, nikaona ni vyema kuzungumza nao na kuamua kuvunja mkataba,” alisema Kotei.

Pia, alisema kwa sasa yupo huru akisaka timu ya kujiunga nayo.

Hata hivyo, tetesi zinadai Kotei yuko katika hatua nzuri za mazungumzo ya kujiunga na Yanga jambo ambalo mwenyewe hakulikanusha wala kulikubali.

“Muda ukishafika na nikishafikia muafaka nitasema wapi nakwenda kucheza. Kwa sasa tuwe na subira,” alisema Kotei.

Katika kipindi cha miezi mitano aliyoichezea Mozyr, Kotei hakuwahi kuanza katika kikosi cha kwanza hata mara moja huku akikaa benchi mara tatu katika mechi 13 ambazo timu hiyo imecheza.

Kotei alitamba vilivyo pindi alipoitumikia Simba kuanzia mwaka 2016 akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili, ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam mara moja lakini pia kuisaidia kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019.

Hata hivyo, baada ya kuondoka Simba, mambo yalianza kumuendea kombo kwani hakupata nafasi katika kikosi cha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo alijiunga nacho na kisha mwezi Disemba, 2019 akavunjiwa mkataba.

Baada ya hapo akajiunga na Mozyr ambayo nayo baada ya miezi mitano tu imeafikiana naye kuvunja mkataba.

No comments: