Na JANETH MUSHI-ARUSHA, MTANZANIA
WAKATI Rais Dk. John Magufuli akitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kumteua Idd Kimanta kushika wadhifa huo, vita ya ubunge inatajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizofanya kutoelewana kati ya viongozi watatu wa mkoa wa Arusha.
Gambo aliyeteuliwa mwaka 2016 baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huoM Felix Ntibenda, kutumbuliwa ni mmoja wa watu waliokuwa wakitajwa kutaka kugombea ubunge wa Arusha mjini kwa tiketi ya CCM.
Baadhi ya viongozi wanaotajwa kuwa ni migogoro na Gambo ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni, ambao pia uteuzi wao ulitenguliwa juzi.
Taarifa zinadai mbali na migogoro na baadhi ya viongozi wenzake pia amekuwa na migogoro na baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa ikiwa ni pamoja na wenye nia ya kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Arusha Mjini.
Gambo anatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaotaka kuwania ubunge katika jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Wengine wanaotajwa ni pamoja na mfanyabiashara Philemon Mollel (Monaban), aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha Calist Lazaro, Edmund Ngemela, Mosses Mwizarubi.
Wakati ikielezwa kuwa migogoro imechangia Gambo na wenzake kung’olewa, imeleezwa kwamba wakati akiwa mkuu wa wilaya mkoani humo, mwanasiasa huyo aliwahi pia kukwaruzana na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Ntibenda.
Mwingine aliyewahi kukwaruzana naye ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Manyara.
Kutokana na migogoro iliyodumu Arusha, viongozi mbalimbali wamefika kwenye mkoa huo kwa nyakati tofauti kujaribu kutuliza hali bila mafanikio.
Hivi karibuni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole, alisema chuki kubwa iliyopo mkoani Arusha kati ya viongozi wa Serikali na chama ni ubunge wa Arusha Mjini.
Polepole ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Arusha na kumtaka Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Zelothe Stephen kumaliza malumbano hayo yaisyokuwa na tija.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwaonya na kuwataka viongozi hao kuacha chuki na kuheshimiana na kusema chuki iliyopo Arusha ni ubunge, kwani kuna watu wana dhamana ya uongozi lakini bado wana tamaa ya ubunge .
“Nawaomba mfahamu kazi hizi tumepewa, hatuna uchaguo lazima tukae pamoja, tupendane na kuheshimiana, tukishindwa hata tufanye kinafiki mambo ya chama yaende,”alisema.
Alisema chuki kubwa iliyopo Arusha ni ubunge, kwani kuna watu wana dhamana ya uongozi lakini bado wana tamaa ya ubunge akisema “hiyo haitawezekana, lazima tuhanganike nao chama hakiwezi kukubaliana na hilo”.
Alisema kuna baadhi ya viongozi waliopewa dhamana za uongozi, lakini hawatosheki kwa kutawaliwa na tamaa za kuta kuacha nafasi hizo na kwenda kugomeba ubunge wakati Tanzania ina wananchi zaidi ya milioni 50 na kati yao wapo wenye sifa za kugombea ubunge.
“Ridhika na kile ulichonacho hasa wale wenye dhamana, mimi sizungumzii wanachama wa kawaida, ndiyo maana watu hawaishi kuleta maneno kuhusu Arusha.
“Chuki zenu mara nyingi ni kwa sababu ya ubunge, na mimi nataka niseme kitu kimoja na hili nikisema mnaweza msilielewe lakini mara zote nongwa hapa nikizisikiliza kuna wale wako mbele (wataka ubunge) halafu kuna wale rafiki zao, sasa matokeo yake unaweza ukajidumbukiza kwenye chukihata hii nafasi uliyonayo ikaharibika, itakapofika kufanya uamuzi (uteuzi wagombea ubunge) unasema yaani huyu ameshajiharibu sana hawezi tena kutujenga umoja.
“Nilishawahi kuwa kiongozi mtumishi wa Serikali lakini nilijitahidi kufanya kazi kwa kuheshimu viongozi wangu hivyo ni vyema viongozi hao wa serikali Arusha kuheshimiana,”alisema.
Licha ya kumwagiza mwenyekiti wa chama hicho mkoa kumaliza tatizo hilo kwa maslahi ya chama, alitoa onyo kwa kamati za siasa za wilaya na mikoa yote nchini zitakazopitisha wagombe ubunge wasio na sifa.
“Hapa si ndiyo tuko kwenye mkoa wetu wa Arusha ni vizuri tukaambiana ukweli, mwenyekiti nilikuwa naomba pia mahusiano ya viongozi wa Serikali hapa mnasemwa vibaya.
“Nimeongea na waziri mmoja anasema hapa hamko vizuri, nimeongea na Katibu Mkuu wa Wizara mama mmoja akasema hapa hamko vizuri, Katibu Mkuu mmojawapo wa wizara mama kaniambia pale iko shida,”alidai Polepole
“Sasa ninyi ndiyo viongozi mnaotoa mwelekeo wa mkoa huu msikubali hilo, wale siyo mashine ni binadamu na viongozi kama sisi, akaniambia wale wameshaitwa wakaambiwa ‘acheni’ lakini bado tunaona moshi unafukuta. Nimelisema hapa kwenye halmashauri kuu kwa unyenyekevu mkubwa jambo hili liishe kabisa,”
KATIBU MKUU CCM
Aidha moja ya video inayosambaa mitandaoni inamwonyesha Katibu Mkuu wa CCM, Dk.Bashiru Alli, anaonekana akisema kuna tatizo Arusha hasa Mkuu wa Mkoa huo (Gambo).
“Kuna tatizo Arusha hasa Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mara pametulia lakini kwa wastani,”
RC,DED NA DC
Katika kile kinachotajwa kuwa mwendelezo wa mgogoro baina yake na Dk. Madeni na Daqqaro, hivi karibuni aliwatuhumu watendaji hao kuwa wanakwamisha utekelezaji wa maelezo ya Serikali.
Gambo alitoa madai hayo akizungumza katika kikao cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG), ambapo alidai tatizo hilo linasababisha kazi za kutatua migogoro ya wananchi kuwa ngumu.
“Hapa watu wamekaa kazi yao ni kufanya mipango ya kumkwamisha Mkuu wa Mkoa kila siku, ukimkwamisha Mkuu wa Mkoa umekwamisha Serikali.
“Hatutaweza na ndiyo maana toka mmeanza mmekuwa hamfanikiwi na nimekuja niwaambie (madiwani) kwa sababu najua ni baraza la mwisho inawezekana mkifunga nisiwepo,”alisema.
Aliwatuhumu viongozi hao kwa kuchangia kuwepo kwa migogoro isiyo ya lazima kati ya Serikali na wananchi na taasisi za dini.
“Tumepata commitment kibao za ofisi ya mkurugenzi hakuna utekelezaji, sasa mimi sijazoea porojo na sijazoea unafiki kwa sababu naamini mtu ukiwa mnafiki wakati ni kijana ukizeeka lazima uwe mchawi a, ujanja ujanja, porojo nisingependa iwe sehemu ya uongozi,” alisema.
Novemba mwaka jana Gambo alisimamisha mchakato wa ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi eneo la Olasiti, kufuatia kuwepo kwa mkanganyiko wa mahali sahihi pakujenga kituo hicho.
Akizungumza katika kikao cha kamati ya shauri ya mkoa huo, Gambo alidai mradi huo ni moja ya miradi yenye tija kwa wananchi hivyo ni vyema ukatelezwa kwa ufanisi na kuagiza Halshamauri ya Jiji la Arusha kusubiri maelekezo zaidi.
RC,DC WAVUTANA KITUO CHA AFYA
Katika hatua nyingine mwanzoni mwa mwaka jana Daqqaro alionyesha kutokuridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Gambo alipozungumzia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya kilichopo Kata ya Muriet.
Sintofahamu hiyo ilijitokeza wakati Gambo akizungumzia ziara ya Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI), Josephat Kandege, kuwa alikagua mabati yaliyoezeka kituo hicho na kudai hayakuwa na ubora.
“Lakini bado pia alivyotembelea Naibu Waziri alikwenda pale na mheshimiwa mkuu wa wilaya wakawa wanasema kuna tatizo la bati, zilizonunuliwa (bati) zina changamoto kidogo,”
“Na sisi tukadhani na kumwambia Katibu Tawala wa mkoa kama kuna hoja imejengwa na ofisi ya mkuu wa wilaya na yeye ni mtu mkubwa anapoonyesha mashaka kwenye eneo fulani,’ alisema Gambo kabla ya kukatishwa na Daqqaro.
Daqqaro alisema “aaaah…mheshimiwa RC usiharibu maneno, mheshimiwa waziri aliagiza, please nikuombe naona unataka kuleta mambo ambayo, no no.”
Baada ya manenio hayo, Gambo aliendelea kwa kusema “aaaaah twende taratibu, aliagiza. Haya basi mheshimiwa Naibu waziri kwa sababu tunao ushahidi hapa wa document, mheshimiwa waziri alivyokwenda pale na mkuu wa wilaya zilitoka hizo allegations (tuhuma).
“Mimi nadhani ofisi ya mkuu wa wilaya ni ofisi kubwa na mtu kama Naibu Waziri naye pia ni mtu mkubwa, anapotoa allegations hizo kama Serikali hatuwezi kuzi ignore (kuzipuuza).
“Nikamwagiza RAS kwamba haiwezekani pakawa na manungu’uniko namna hiyo halafu Serikali kwenye ngazi nyingine, ikanyamaza tu kimya, kama kinachosemwa hakina tija tumeelekeza TBS makao makuu waje hapa waende kwenye kile kituo wakahakiki kama kuna uhalisia kwenye jambo hili au hakuna uhalisia kwenye jambo hili.”
DK.MADENI
MTANZANIA JUMAPILI ilimtafuta kwa njia ya simu Dk. Madeni ambaye alijibu “sina la kusema” na kisha kukata simu huku simu ya Daqqaro ikiwa haipatikani.
TAMISEMI
Juni 10 mwaka huu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suleiman Jafo, Katibu Mkuu Joseph Nyamhanga na baadhi ya viongozi waliwakutanisha watendaji hao (Gambo, Daqqaro na Dk. Madeni).
Watendaji hao walikutanishwa katika kikao kilichofanyika ofisi za Tamisemi jijini Dodoma ambacho kilikuwa na lengo la kuimarisha uongozi na utawala bora katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment