ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 14, 2020

Man City kushiriki UEFA kama kawaida



NYON, USWISI, MTANZANIA

TIMU ya Manchester City imefanikiwa kushinda rufaa yao ya kutoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka miwili, hivyo sasa watashiriki kama kawaida.

Februari mwaka huu timu hiyo ilifungiwa kushiriki michuano hiyo mikubwa barani Ulaya kwa misimu miwili kutokana na tuhuma za kuvunja sheria za matumizi ya fedha michezoni.

Lakini Manchester City waliweka walidai hawakufanya kosa lolote, hivyo walipelaka rufaa yao katika Mahakama ya Michezo (CAS), ambapo walianza kuisikiliza tangu mwezi uliopita.

Jana asubuhi CAS ilitoa taarifa baada ya kufanya uchunguzi wa kutosha kwa kipindi chote hicho na kufikia hatua kwamba timu hiyo ipo huru kushiriki.

“Ukiukwaji mwingi ulioripotiwa na Chumba cha Uamuzi cha CFCB (Baraza la Udhibiti wa Fedha) labda haukukamilisha ripoti yao au muda wa kufanya hivyo ulipita.

“Kutokana na hali hiyo inakuwa ngumu kwa klabu ya Manchester City kufungiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ilivyoripotiwa hapo awali,” walisema CAS.

Hata hivyo, mara baada ya CAS kutoa taarifa hiyo, Manchester City walitumia ukurasa wao wa habari na kuwapa taarifa mashabiki zao kuwa watakuwepo kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

“Wakati Manchester City na washauri wake wa kisheria wakiwa bado hawajachunguza uamuzi kamili wa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), lakini klabu inapenda kuwashukuru wanachama wa jopo kwa bidii yao na mchakato unaofaa waliosimamia,” waliandika Man City.

UEFA walichukua hatua hiyo ya kuifungia Man City mara baada ya kuvuja kwa taarifa Februari 14 kutoka gazeti la nchini Ujerumani kwamba timu hiyo imevunja sheria za matumizi ya fedha kuanzia mwaka 2012 hadi 2016 na wakatakiwa kulipa faini ya pauni milioni 26.9.

Manchester City walikuwa na hofu ya kuwapoteza wachezaji wake endapo kifungo hicho kingepita. Miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wanatajwa kuwa wangeweza kuondoka mwishoni mwa msimu huu kutokana na hali hiyo ni pamoja na kiungo wao Kevin De Bruyne mwenye umri wa miaka 29, Raheem Sterling na wengine.

Katika msimamo wa Ligi nchini England, Manchester City wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 72, wakati huo Liverpool ambao ndio mabingwa wana pinti 93 baada ya kucheza michezo 34.

No comments: