Monday, July 27, 2020

Mgombea udiwani aangusha kibuyu akiomba kura



ABDALLAH AMIRI– IGUNGA

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mmoja wa wagombea wa udiwani Kata ya Sungwizi, Katambi Sospeter alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuagusha kibuyu chenye dawa za kienyeji wakati akiingia kwenye ukumbi wa mkutano wa kura za maoni za CCM.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 5 asubuhi wakati mgombea huyo alipokuwa akipandisha ngazi ili kuingia kwenye jengo la ukumbi wa mikutano, ndipo kibuyu hicho kilichomoka kutoka kwenye mfuko wake wa suruali mbeole ya wajumbe wa mkutano huo.

Baada ya kibuyu hicho cha mgombea huyo ambaye alijikuta akipigwa na bumbuwazi na kushindwa kusema lolote.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano mkuu wa kata hiyo, Theresia Bleck, alilazimika kumwita mgombea huyo lakini alishindwa kukiokota na badala yake mjumbe huyo alikiokota na kumkabidhi mgombea huyo.

Kutokana na hali hiyo askari wawili wa Jeshi la Akiba (Mgambo), alimuhoji mgombea huyo kitendo cha kuwa na kibuyu chenye dawa mkutanoni.

Mgombea Katambi alikiri kuwa hicho kibuyu ni cha kwake huku akisema yeye amezaliwa mapacha hivyo utaratibu inatakiwa awe na kibuyu cha dawa wakati wote.

Pamoja na kujieleza kwa mgambo hao walimkatalia kuingia na kibuyu na kutakiwa kwenda kujieleza na akimaliza atakabidhiwa lakini aligoma kufanya hivyo.

“Jamani ndugu zangu mgambo na wewe mwandishi wa habari naomba mniache mimi niingie na kibuyu changu, ngoja niwape fedha kidogo za maji na vocha haya ni maisha ndugu zangu,” alisema mgombea Katambi.

Aidha pamoja na maombi hayo mgambo hao waligoma kupokea fedha baadaye Katambi aliamua kukipeleka kibuyu hicho nyumbani na kurudi kupiga kura za maoni.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Sungwizi, Emmanuel Mpya alithibitisha mgombea huyo kuangusha kibuyu cha dawa kabla hajaingia kupiga kura za maoni huku akisema kitendo hicho hakikumfurahisha.

Aidha alitoa wito kwa mgombea huyo kutorudia tabia hiyo ya kuingia na dawa ya kienyeji kwenye vikao kama hivyo vya kura za maoni huku akimwamuru kuingia bila kibuyu hicho cha dawa katika jengo hilo.

Baada ya kutii maelekezo hayo wajumbe walipiga kura za maoni ambapo msimamizi Ramadhani Omari alitangaza matokeo ambapo Njeri Ibrahim alipata kura 21, Katambi Sospeter aliyedondosha kibuyu cha dawa alipata kura 22 na diwani aliyemaliza muda wake, Matikito Gaspar aliongoza kwa kura 62.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake