Thursday, July 23, 2020

TCRA Zanzibar yaeleza mchango wa mawasiliano kwenye uchumi wa nchi



Na KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR , MTANZANIA

MKUU wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ofisi ya Zanzibar, Esuvatie Aisa Masinga, amesema kukua kwa uchumi nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta ya mawasiliano kupitia mafundi simu waliopo.

Esuvatie alisema hayo alipofungua semina ya siku moja kwa mafundi simu wa Zanzibar iliyoandaliwa na TCRA, katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni mjini Unguja.

Aidha alisema kila kitu ambacho kimepata mafanikio kuna hatua mbali mbali zimepitia ambazo wakati mwengine zinakuwa fursa adhimu kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema TCRA ina dira yake, ambayo itaweza kufikia kiwango chenye hadhi ya kimataifa na kwa hali hiyo wameona na wao ni muhimu katika kufikia huko.

“TCRA imekuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa Tanzania, jitihada hizi sio za mamlaka tu, bali zilianza kwenu nyinyi mafundi simu ambao ni wadau wakuu wetu, tumefanikiwa kutokana na ngumu yenu.

“Endeleeni kutuunga mkono na sisi kama wasimamizi wenu hatutowaangusha, naamini huu ni mwanzo mwema sio hata miaka minne mengine ukasikia tumeingia hatua ya juu zaidi kiuchumi, sina hofu na hilo kwani safari moja huanzisha nyengine,” alisema Esuvatie.

Mhandisi wa Mawasiliano kutoka TCRA Makao Makuu na fundi simu wa zamani, Baluhiye Kadaya alisema kuwa teknolojia ya simu za mkononi imekuwa baada ya kila mmoja kubaini fursa zilizomo ndani yake.

Alieleza kuwa sasa kuna matumizi makubwa ya simu kuliko vitu nyengine vya elektroniki kutokana na urahisi wake kwenye matumizi.

Pia aliwataka mafundi hao kujaribu kulinda kazi hiyo na kutokuwa tayari kuruhusu wachache kuwaharibia.

Alisema kuwa ni lazima watu waelewe kuwa kazi hiyo inalipa, hivyo inahitaji kulindwa ili isiharibiwe, sambamba na kukemea mafundi hao kubadilika na kujaribu kuwa na mikataba na wateja wao ili kuondosha malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake